Marekani, Kuanzia muvi ya “Straight Outta Compton” hadi andiko la kitaaluma (dissertation) la Kristen Bowen, Chuo Kikuu cha North Carolina. Documentaries za “In The Dark”, “Surviving Diddy” kisha “Freak Off Parties”. Halafu kitabu “Mercedes Ladies” cha Sherri Sher.
Kila moja inatosha kujenga picha ya mwanzo wa mwisho wa binadamu ambaye alipata kuonekana ni kila kitu katika ulimwengu wa burudani, Sean Combs “Diddy”, zamani “P Diddy”. Miaka ya 1990, aliitwa “Puff Daddy” au simply “Puffy”.

Muvi ya Straight Outta Compton, inasimulia maisha halisi ya vijana watatu wenye vipaji na fedha kutoka Compton, California; Eazy E, Ice Cube na Dr Dre. Walikuwa memba wa Hip Hop crew ya N.W.A (Niggaz Wit Attitudes). “Straight Outta Compton” ni albamu yao ya kwanza na iligonga platinum mwaka 1988.
Ndani ya movie ya Straight Outta Compton, kilichowasilishwa kama uhudika wa Eazy, Cube na Dre, ndicho kimeandikwa na Kristen Bowen katika dissertation (tasnifu) yake yenye jina “Sexual Violence, Black Survivors, and Moving Beyond Resilience.”
N.W.A, walipofanya vizuri sokoni kupitia albamu yao, utawaona wakiangusha house parties za nguvu. Humo ni pombe, wanawake na bangi. Mapenzi kwa makundi. Mastaa watatu katikati ya msitu wa wanawake. Uchafu wa kila aina unafanyika. Huoni thamani ya mwanamke zaidi ya kuwa chombo cha starehe.

Koridoni, gereza alilowekwa Diddy
Wanawake wote ni weusi. Hili linafafanuliwa na Kristen katika tasnifu yake chuoni North Carolina, kwamba wanawake weusi kutumikishwa kingono ni mnyororo wa kihistoria tangu zama za utumwa. Kisha, utamaduni maarufu (popular culture), mwanzoni ulitawaliwa na Wazungu kibiashara.
Kutokana na hali hiyo, Wazungu waliwazubaisha mastaa Weusi kwa kuwaandalia parties zenye pombe na wanawake. Fedha zao nyingi zilipotea humo. Ndicho kinachoonekana kwenye muvi “Straight Outta Compton”, na ni moja ya sababu za kusambaratika kwa N.W.A mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Parties hizo za pombe na wanawake weusi, zinashabihiana na Freak Off Parties za Diddy, vilevile mnyororo wa mastaa Weusi, kukumbwa na kashfa nyingi za kuwanyanyasa kingono wanawake Weusi, hadi ubakaji. Diddy akaunga orodha. Hatimaye yupo nyuma ya nondo
Mwaka 1993, Rapa Tupac Shakur, alitoa ngoma “Keep Ya Head Up”, ambayo iligeuka wimbo wa kila mwanamke Mweusi. Katika single hiyo, Tupac anawashukia vikali wanaume weusi, tabia yao ya kubaka wanawake. Alipokuwa hai, Tupac alisema, aliandika wimbo kwa sababu vitendo vya ubakaji kwa wanawake Weusi vilikuwa vingi na wabakaji ni wanaume Weusi.
Oktoba 1999, ikiwa ni miaka mitatu tangu kifo cha Tupac, ulitolewa wimbo mwingine wa rapa huyo, unaoitwa “Baby Don’t Cry”, ambao ni sehemu ya pili ya “Keep Ya Head”, akifikisha ujumbe jinsi wanawake Weusi wanavyonyanyaswa kingono kwa kubakwa hovyo na wanaume Weusi.
Hatima ya Diddy
Diddy, mwana-Hip Hop tajiri ambaye mwishoni mwa miaka ya 1990 hadi katikati ya muongo wa pili wa miaka ya 2000, alitambulika kama mwanamuziki mwenye fedha nyingi zaidi duniani, kabla ya kupitwa na Jay Z, kisha Kanye West na Rihanna.
New York finest, Diddy, ni mtetezi hasa wa jumuiya ya watu Weusi. Alianzisha kampeni ya kuyakweza mafanikio ya watu Weusi, aliyoiita “Black Excellence”. Zaidi, Diddy, alikuwa kiunganishi cha watu Weusi maarufu na mpatanishi palipo na migogoro. Hata hivyo, hivi sasa ni kama anaielekea omega!
Diddy, yupo mahabusu kwenye magereza ya MDC (Metropolitan Detention Centre), Brooklyn, New York (pichani). Anashitakiwa kwa makosa mengi ya ukatili wa kingono kwa wanawake. Alikamatwa Septemba 16, 2024, Manhattan, New York.

Gereza la ‘Metropolitan Detention Centre’ alilowekwa Diddy
Kabla ya kukamatwa, Machi 25, 2024, polisi walivamia nyumba za P Diddy zilizopo Los Angeles, California na Miami, Florida. Katika uvamizi huo wa kiupelelezi, polisi walinasa makopo 1,000 ya mafuta ya watoto, vilainishi na dawa za kulevya. Vyote hivyo vinatajwa kuwa vitendea kazi vyake vya ukatili wa kingono.
Diddy, binadamu mwenye ufahari mkubwa wa kimaisha, hivi sasa analala kwenye kichumba cha futi nane kwa 10, analalia kitanda cha chuma chenye upana wa meta moja na nusu, halafu godoro halina mto. Akitaka kunyoosha miguu chumbani, atatembea kwa hatua tano tu. Hakuna hata kitabu cha kusoma.
Maisha ya mansions za baharini (waterfront), mahekalu makubwa yenye kila starehe. Massage za kila siku kwenye vyumba maalumu, picnics baharini kwa kutumia yachts zake za kifahari, misele kwa ndege zake binafsi, matembezi kwa magari ghali duniani na mavazi ya kikwasi. Vyote hivyo hana uhuru navyo. Kwa sasa, analazimika kupaita MDC nyumbani, akisubiri hatima yake.
Akiwa MDC, Diddy analazimika kuchangia mahabusu na haramia hatari wa dawa za kulevya kutoka Mexico, Ismael Zambada Garcia “El Mayo” na tapeli wa fedha za kidigitali (cryptocurrency), Bankman Fried.
MDC pia walishakaa, Rapa Fetty Wap na mfalme wa R&B duniani, R Kelly, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 20, baada ya kukutwa na hatia ya kuwatumikisha watoto kingono.
Gereza la MDC, linatajwa kuwa hatari kwa wafungwa na mahabusu.
Vurugu za kupigana pamoja vifo hutokea. Juni 2024, mshitakiwa wa kesi ya bunduki, Uriel Whyte, aliuawa kwa kuchomwa kisu. Julai 2024, mfungwa Edwin Cordero, alifariki dunia akipigana. Januari 2019, gereza hilo lilipata hitilafu ya umeme, wafungwa na mahabusu wakakaa gizani na kwenye joto kali kwa wiki nzima.
Ndani ya miaka mitatu iliyopita, watu watatu wamejiua kwenye gereza la MDC. Hali hiyo ndiyo ambayo imekuwa ikisababisha wanasheria wa Diddy, walalamike mteja wao kupelekwa MDC, kwa sababu wanaona usalama wake ni mdogo.
Diddy alivyosakwa
Novemba 23, 2023, mwanamuziki Cassie Ventura, alifungua mashitaka Mahakama ya Wilaya, Manhattan, dhidi ya Diddy, akidai kipindi wakiwa wapenzi kati ya mwaka 2007 mpaka 2018, galacha huyo wa Hip Hop, alimfanyia vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia. Kesi hiyo, walimalizana nje ya mahakama.
Siku hiyohiyo (Novemba 23), mwanamke mwingine, Joi Dickerson, alifungua mashitaka kwenye Mahakama ya Wilaya, Manhattan, akidai Diddy alimleweshwa kwa dawa za kulevya, akambaka, akamrekodi video za ngono na kusambaza.
Desemba 6, 2023, mwanamke aliyetambulika kwa jina la Jane Doe, alifungua mashitaka Mahakama ya Wilaya, Manhattan, akidai Diddy akishirikiana na wanaume wengine wawili, walimlewesha kwa dawa, kisha wakamsafirisha kutoka Detroit hadi New York, walipombaka ndani ya studio za Bad Boy Entertainment.
Februari 26, 2024, prodyuza Rodney Jones “Lil Rod”, alifungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Kusini, New York, amkimshitaki Diddy, kumlazimisha kutumia dawa za kulevya pamoja na kufanya mapenzi na wanawake makahaba.
Machi 25, 2024, nyumba kadhaa za Diddy, zilizopo Los Angeles na Miami, zilivamiwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Ndani. Aprili 4, 2024, Grace O’Marcaigh, alifungua kesi Mahakama ya Kaunti ya Los Angeles, akidai kubakwa kwenye Yacht na mtoto Diddy, Christian Combs “King Combs”.
Grace alidai mahakamani kuwa Diddy ndiye aliyemsaidia King Combs kumbaka, kisha alimhonga fedha dereva wa Yacht, anyamaze. Mei 23, 2024, mwanamke April Lampros, alifungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Kusini, New York, akidai kati ya mwaka 1990 na 2000, Diddy alimfanyia mashambulizi mengi ya kingono.
Mei 22, mwanamitindo wa zamani, Crystal McKinney, alifungua madai mahakama ya shirikisho, Manhattan, akimtuhumu Diddy kumlewesha kwa dawa za kulevya na kumfanyia shambulizi la ngono, studioni kwake, New York, mwaka 2003.
Juni 2024, Diddy alikutwa na hatia mahakamani ya kumlewesha kwa dawa za kulevya na kumshambulia kingono, Derrick Smith, 51. Mahakama iliamuru Diddy amlipe Smith fidia ya dola za Marekani 100 milioni (Sh270 bilioni). Hata hivyo, mawakili wa Diddy wamekata rufaa.
Septemba 11, 2024, mrembo Dawn Richard, alimshitaki Diddy, Mahakama ya Wilaya ya Kusini, New York, akimtuhumu kumfanyia mashambulizi ya kingono na kumuumiza kisaikolojia, kipindi alipokuwa anashiriki kipindi cha televisheni cha Making the Band 3, kilichoanzishwa na Diddy.
Pigo kuu kwa Diddy
Diddy mwenyewe na wanasheria wake, walikuwa wakikanusha kila tuhuma, ikiwemo ya Cassie. Mei 18, 2024, Diddy alipigwa bomu zito, unaweza kuliita “coup de grace”, yaani pigo la kusimamisha moyo. Video akimpiga na kumburuza Cassie, ziliwekwa mtandaoni.
Video hizo, zilirekodiwa kupitia kamera za usalama (CCTV Camera), zinamwonesha Cassie akiwa amebeba begi akitembea kwa haraka, kisha Diddy anatokea kwenye korido akimkimbiza, alimpofikia, alianza kumpiga kwa ngumi na mateke, kisha akamburuza kumrudisha chumbani. Ni tukio la Machi 2016, Hoteli ya InterContinetal, Los Angeles.
Mei 19, 2024, Diddy alijitokeza kuomba msamaha. Pamoja na hivyo, tukio la kumpiga Cassie, lilionekana kumfikisha pabaya. Wengi walitabiri kuwa iliwadia tamati ya godfather wa Bad Boy Entertainment. Hatimaye, sasa anaishi kwa kijiminya kwenye chumba kidogo chenye nondo nzito, ndani ya gereza la MDC.
Mlinzi wa zamani wa Diddy, Gene Deal, amesema mara kadhaa kuwa tabia ya boss huyo wa Rivolt TV, kwa kiasi kikubwa imechangiwa na mentors wake wawili, Russell Simmons na marehemu Andre Harrell. Russell, alipoona anasumbuliwa na tuhuma nyingi mashambulizi ya ngono kwa wanawake, alikimbilia Bali, Indonesia, anakoishi.
Machi 2024, Russell alitumiwa hati ya mashitaka dhidi yake kutoka Marekani, ambayo aliipokea akiwa Bali. Russell hajawahi kurejea Marekani kuitikia wito. Hivi sasa, Russell hamiliki mali yoyote Marekani, aliuza akahamia Bali.
Kwamba michezo ya kubaka wanawake na hata kuwageukia wanaume, kwa mujibu wa Deal, Diddy amejifunzwa kutoka kwa Russell na Harrell, ambaye ni bosi wa zamani wa studio ya muziki ya Uptown Records. Kupitia Uptown, Harrell alimwajiri Diddy na kumkuza kimuziki, kabla hajaanzisha label yake, Bad Boy Entertainment.
Kufikishwa mahakamani kwa Diddy bila shaka ni kilele cha docuseries za In The Dark na Surviving Diddy, bila kuacha mahojiano mfululizo kuhusu Freak Off Parties. Inatafsiri anguko la mbuyu katika biashara ya muziki. Binadamu ambaye amechonga barabara za wengi; Notorious BIG, Craig Mack, Mase, Fabulous, 112, Faith Evans, nimetaja wachache.