
Liverpool. Liverpool imeendelea kuonyesha ubabe wake kwenye Ligi Kuu England baada ya kuichapa Wolves mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Anfield.
Ushindi huu umeifanya Liverpool kuendelea kujidhatiti kileleni ikiwa na pointi 60, saba mbele ya Arsenal inayoshika nafasi ya pili baada ya kila moja kucheza michezo 25.
Luis Diaz ambaye amekuwa kwenye kiwango cha juu kwa siku za hivi karibuni alikuwa wa kwanza kuifungia Liverpool bao katika dakika ya 15 tu ya mchezo baada ya kuyatumia vyema makosa ya mabeki wa Wolves.
Dakika saba kabla ya mapumziko Mohamed Salah aliifungia Liverpool bao la pili kwa mkwaju wa penalti na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0, likiwa ni bao la 23 kwa mshambuliaji huyo.
Dakika ya 67, Matheus Cunha alifungia timu yake bao moja hali ambayo ilibadili kabisa mchezo huo baada ya Wolves kupata nguvu na kushambulia kwa nguvu lango la Liverpool ambao walitumia muda mwingi kulinda ushindi wao.
Wolves wameendelea kuwa kwenye nafasi mbaya baada ya kuwa katika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 19 tu baada ya michezo 25.