Dar es Salaam. Nyota wa muziki nchini Diamond Platnium amesema anaongoza kwa kuwaandikia nyimbo wasanii wa lebo yake tofauti na wengi wanavyodhani huko nje.
Diamond amesema hayo kukiwa na minong’oni kutoka kwa baadhi ya watu wakidai msanii huyo husaini wasanii kwenye lebo yake ili wasaidie uamuandikia nyimbo.
“Watu wengi nje wanaimani yao kwamba mimi ninasaini wasanii ili waniandikie nyimbo. Mimi nimeandika nyimbo za wasanii wengi ambazo nyie hamjui. Wasanii wa Wasafi kila mtu akija hapa kati ya mimi na yeye nani kamuandikia mwenzie nyimbo nyingi watawaambia.

“Hata wengine sio wa Wasafi hata wenyewe huwa wanazungumza. Mimi siwezi kuona wimbo wako haukosawa halafu nikakuacha tu nitakusaidia. Mimi uwezo wangu umetokana na kuandika yaani mimi kama mwanamuziki nikishika peni naweza nikakuandika wimbo wowote, Bolingo, R&B, Kibao Kata, Hiphop, Amapiano na kila muziki na jua niandike vipi,” amesema Diamond.
Hata hivyo, Diamond amegusia baadhi ya wasanii kutozwa pesa wanapotaka kujitoa kwenye lebo walizosainiwa. Ambapo kwa upande wake amesema hufanya hivyo endapo msanii asipokuwa na heshima.

“Ukiona mtu nimemtoza hela ujue huyo amenikosea adabu, mimi sitegemei hela ya wanamuziki wa lebo katika mapato yangu. Mimi nawachukulia kama ndugu zangu familia yangu, kuna mtu akinikosea naumia na ndio maana unakuta mtu kama Mbosso mimi nilimwambia asinilipe hata shilingi kumi,”amesema Diamond.

“Kinachotokea msanii akitoa kwenye lebo yetu ni ngumu kupotea kwa sababu pale ni shule tunawafundisha kila kitu. Namna ya kujibrand, kuandika, kudansi, biashara ya muziki na kila kitu kuhusu muziki,”