Diamond, Harmonize kuweka alama miaka 22 ya Mr Blue kwenye gemu

Dar es Salaam. Msanii wa muziki nchini, Mr.Blue ambaye mwaka huu anatimiza miaka 22 kwenye kiwanda cha burudani, ametangaza kuachia nyimbo 22 kama zawadi kwa mashabiki wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 2, 2025 Mr. Blue amesema nyimbo hizo atazitoa kwa awamu, akianza na video za nyimbo nne zitakazotoka leo.

“Nilianza mwaka 2003 kutoa ngoma kama msanii Mr.Blue na huu ni mwaka 2025. Kwa hiyo kama umeona hapo kwa hesabu za haraka ni miaka 22 nimekuwa nikifanya hiki kitu. Kwahiyo siku zimeenda na nikafikiria kitu gani nifanye. 

“Namshukuru Mungu nimepata jibu nikaona nitoe nyimbo 22 ambazo ni kama kuwashukuru mashabiki kwa kunisapoti kwa miaka 22. Nyimbo hizo nitazitoa kwa awamu ambapo leo nitatoa nyimbo nne kwanza,” amesema mr.Blue

Katika ngoma hizo 22 anazotarajia kuachia Mr.Blue amesema  mashabiki watarajie kukutana na kolabo akiwa na wasanii wakubwa kama Harmonize, Diamond Platnumz n.k

“Muwategemee wasanii wote kwa miaka hii 22, nimepata bahati ya kufanya kazi na wasanii wa kileo na wasanii wa zamani, kwa sababu mimi nimelelewa na wasanii kama kina Afande Sele, Juma Nature TID na Dully Sykes.Pia, nimekutana na wadogo zangu wengine ndio hawa kina Diamond. Nimekuwa ni mtu mwenye bahati kufanya kazi na vizazi vyote hivi, hivyo muwategemee,”amesema.

Ameongezea kwa kusema zawadi ya nyimbo 22 ameona inawafaa mashabiki wake.

“Kuna wakati mwingine sitoi nyimbo hata miaka mitano lakini watu bado wananiita nikaimbe kwenye shows kwa hiyo ni upendo mkubwa. Ukienda kwa mtumishi wa Mungu zawadi atakayokupa ni kukuombea dua sasa mimi ni msanii nikajiuliza niwape watu zawadi gani, wamenisapoti sana mimi nimetokea kwenye maisha ya kimasikini sana, hivyo nimeona nije na zawadi hii ya nyimbo 22,” amesema Blue. 

Hata hivyo, Mr. Blue ameitambulisha rekodi lebo yake inayoitwa ‘Blue Record’ ambayo itatambulisha wasanii na kutoa nafasi kwa watu wenye vipaji vya kuimba.

“Kama kuna msanii anataka kurekodi aje, na pia tutatoa wasanii kupitia Blue Rekodi kama wengine wanavyofanya. Tumeona Diamond, Harmonize na Alikiba,” amesema.

Blue amesema lebo hiyo haitoishia kusaini wasanii wa hip-hop pekee, bali hata wale waoimba lengo ikiwa ni kusapoti aina zote za Muziki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *