Diamomd anapita njia aliyoitumia kwa Zari?

Dar es Salaam. Ndilo swali la wengi baada ya Diamond Platnumz kukumbwa na kashfa mpya ya usaliti wa uhusiano wake, kashfa inayoteka mazungumzo mtandaoni kwa sehemu kubwa na sasa inangojewa kuona ipi itakuwa hatima yake.

Hata hivyo, tayari Diamond amejitokeza kwa umma na kukiri makosa yake lakini akitupa lawama kwa yule aliyemtaja kama mpenzi wake wa zamani kwa madai  ya kuwa ndiye amesambaza video zao mtandaoni za kipindi wapo wote.

“Na mwanamke huyo pia niliachana naye takribani miaka miwili sasa, lakini pia nilimueleza mwenzangu niliyenaye [Zuchu] na tukasameheana na kuanza maisha mapya,” ni sehemu ya ujumbe mrefu aliandika Diamond katika Insta Story.

Hatua hiyo ilikuja siku chache tangu kupita siku ya wapendanao ambapo Diamond alimtumia Zuchu ujumbe uliojaa maneno matamu ya mahaba akisema kati ya wanawake wote aliowahi kuwa nao, yeye ndiye anampenda zaidi.

Utakumbuka Diamond ameshawahi kuwa na uhusiano na warembo kadhaa akiwemo Penny, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto, Zari The Bosslady na Tanasha Donna ambaye walishirikiana katika wimbo uliofanya vizuri, Gere (2020).

Zari kutokea Uganda aliyezaa na Diamond watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016), katika siku ya wapendanao 2018 alitangaza kuachana na mwanamuziki huyo zikiwa ni siku chache tangu kusambaa kwa picha na video akikumbatiana na Wema.

“Nimeamua kusitisha uhusiano wangu na Diamond, tumetengana kama wapenzi lakini si kama wazazi, nitawafundisha wanangu wanne  kuwaheshimu wanawake kila wakati na kumfundisha binti yangu maana ya kujiheshimu,” alisema Zari kupitia Instagram.

Uamuzi huo wa Zari ulikuja takribani miezi mitano tangu Diamond kukiri kuzaa na Hamisa baada ya tetesi za muda mrefu, alikuwa akikwepa jambo hilo kutokana na wakati huo alikuwa na Zari ila ikafikia hatua ikabidi akubali yaishi.

Zari hakuwa mwanamke wa kwanza kuachana na Diamond kwa madai ya kukosa uaminifu, mwingine ni Penny aliyechukua uamuzi kama huo kufuatia kusambaa picha mtandaoni zikimuonyesha Diamond akiwa Hong Kong  na aliyekuwa mpenzi wake, Wema.  

“Watu wanaachana kwa sababu nyingi, nilihisi kwamba nahitaji kumpa nafasi, wote ni vijana na wakati mwingine tunahitaji nafasi kugundua vitu vipya, kuona kipi hasa unachokihitaji katika maisha, hivyo nilihisi wote tulihitaji hicho, hivyo nikampa nafasi na mimi kuchukua nafasi,” alisema Penny.  

Zuchu naye amewahi kutangaza mara kadhaa kuachana na Diamond, mara ya mwisho alifanya hivyo Novemba 2024.

“Baada ya miaka mitatu ya mahusiano, mimi na Naseeb [Diamond] tumeamua kwa amani kuachana, huu ni uamuzi wa pamoja kutoka pande zote mbili,” alisema Zuchu.

Hata hivyo, baada ya kauli hii walirudiana na kutoa wimbo, Wale Wale (2024) ukiwa ni wa tano kwa wawili hao kushirikiana baada ya kutoa Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022) na Raha (2024).

Kwa miaka mingi Zuchu kupitia tungo zake amekuwa akijisifia kumshika vilivyo mpenzi wake, mathalani katika wimbo wake, Fire (2022) kutoka katika mradi wake wa 4:4:2, anasema; Mkubwa kwenu ninyi ila kwangu hana kauli!.

Ikumbukwe uhusiano wa Diamond na Zuchu ulianza kwa tetesi nyingi ambazo walizikanusha ikiwa ni miezi kadhaa tangu msanii huyo kuachana na Tanasha Donna kutokea Kenya ambaye walijaliwa kupata mtoto mmoja, Naseeb Jr (2019).