
Mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji amewataka mashabiki wa timu hiyo kuamini kuwa itapata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano dhidi ya Al Masry ya Misri, Aprili 9, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ambayo yataipeleka hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika licha kufungwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ugenini.
Matokeo ya mchezo uliopita uliofanyika katika Uwanja wa Suez, Misri yanailazimisha Simba kuhakikisha inapata ushindi wa angalau mabao 3-0 ili isonge mbele na kutinga nusu fainali.
Dewji alisema kuwa wana imani kubwa ya kikosi chao kupata ushindi wa idadi kubwa katika mechi ya marudiano nyumbani hivyo mashabiki wa Simba wanapaswa kutokuwa na presha kwani wana timu bora ambayo itawapa furaha.
“Hakuna kitu kitamu kama kupata kitu wakati ukiwa hauna matumaini. Ukiwa na matumaini furaha inakuwa kiasi kwa hiyo tunawaomba wajitokeze kwa wingi ili tuweze kuwapa furaha.
“Tulicheza mpira mzuri kwa bahati mbaya hatukuwa na bahati lakini kwa nyumbani hapa Mungu akijalia tutacheza vizuri na tutarudisha magoli. Wachezaji tumeshaongea nao na wao wenyewe wanaelewa kwamba tumefungwa kwa bahati mbaya lakini kila mchezaji anasema kwamba atahakikisha anacheza mara mbili ya zaidi alivyocheza kwenye mechi ya kwanza ili tuweze kupita,” alisema Dewji.
Dewji alisema kuwa Al Masry itakutana na Simba ya tofauti Dar es Salaam na hakuna namna itaepuka kipigo kwenye mechi hiyo huku akianika sababu tatu zinazompa imani hiyo.
“Kwanza timu zote za bara la Afrika zinauogopa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwamba hatoki mtu salama kwa hiyo wanakuja na hofu hiyo na pili hiyo timu waliona tulivyocheza. Uwanja wa Mkapa ni mkubwa kidogo kuliko uwanja wao hivyo hapa kutanuka inakuwan ni vizuri zaidi.
“Lakini pia wale walibebwa na mwamuzi kwenye mechi ya kwanza. Kwa Mkapa kinachofanya timu ishinde ni wapenzi na mashabiki. Sisi tunazingatia zaidi mambo ya ndani ya uwanja na hatuchezi mchezo nje ya uwanja. Tunatafuta haki na kila siku Mungu anapenda mtu anayependa haki,” amesema Dewji.
Kwa upande wake meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa suala la wao kuwatoa Al Masry ni jukumu wanalolimudu.
“Mara baada ya kuwasili, moja kwa moja tunaelekea kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wetu wa marudiano, Aprili 9. Sisi hatujapotza mchezo kwa sababu bado tuna nafasi kubwa ya kufuzu kwenda hatua inayofuata kwa maana ya nusu fainali.
“Matokeo ya kule Suez Misri, hayajatutingisha hata kidogo na wala hayajatuyumbisha hata kidogp. Nafasi kuvuka bado tunayo na hii ngoma bado mbichi sana na tangu mwanzo tulisema hii tunavuka. Tunafahamu ni nini tunapaswa kufanya ili Simba iende fainali. Tumeshavuka viunzi na vigingi vikubwa. Katika timu ambayo inaongoza kutoa vipigo Afrika ni Simba.
“Wachezaji wamesema hii tunavuka. kila mmoja ambaye nimekuwa nikizungumza naye ananiambia Ahmed usiwe na mashaka, wewe ita Wanasimba sisi tunajua cha kufanya. Na Al Masry atakuwa Mwarabu wa kwanza kuwa mfano. Kiu tuliyokuwa nayo ni kumchakaza Mwarabu,” amesema Ally.