Dereva teksi akamatwa akituhumiwa kumuua abiria miaka tisa iliyopita

Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Omari Mwanamtwa (60), dereva taksi, mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kumuua abiria wake Ulumbi Stephano (62) aliyekuwa na ulemavu wa miguu.

Mwanamtwa anadaiwa baada ya kufanya mauaji hayo miaka tisa iliyopita alitoroka.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Alex Mkama amewaeleza waandishi wa habari leo Alhamisi, Machi 6, 2025 kuwa tukio hilo la maujaji lilitokea Machi 2016 katika eneo la Kasanga, Manispaa ya Morogoro na mpaka sasa mwili wa marehemu haujapatikana.

“Huyu mama mwenye ulemavu ambaye enzi ya uhai wake muda mwingi alikuwa akitumia teksi ya mtuhumiwa, ghafla alipotea na baada ya uchunguzi wa polisi teksi hiyo ilikutwa imetelekezwa kwenye kituo kimoja cha mafuta ikiwa na damu.

Kutokana na hali hiyo, uchunguzi wa kitaalamu uliofanyika ulibaini damu iliyokutwa kwenye ile teksi ilikuwa ya Ulumbi Stephano,” amesema.

Kamanda huyo amesema teksi hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na mtuhumiwa, ni mali ya Mayasa Hashimu, ofisa elimu mstaafu na mkazi wa Tanga.

Amesema kwa sasa mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na uchunguzi wa polisi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Akizungumzia namna mtuhumiwa huyo alivyokamatwa, Kamanda Mkama amesema ni baada ya kupenyezewa taarifa kutoka kwa raia wema wanaofahamu tukio hilo, ambao walimuona nyumbani kwake na baada ya taarifa hizo polisi waliweka mtego na kumkamata.

“Hili tukio lilitikisa hapa Morogoro na huyu jamaa tayari tulishatangaza kuwa tunamtafuta, hivyo aliporudi tu nyumbani kwake watu wakatueleza na sisi tukafanyia kazi taarifa hizo, hatimaye tukafanikiwa kumkamata,” amesema Kamanda Mkama.