Denzel Washington sasa ni mtu mwingine kabisa 

Marekani. Mkongwe wa filamu Marekani, Denzel Washington, 69, amesema  amefanya uharibifu mkubwa katika mwili wake kipindi alichokuwa akitumia dawa za kulevya na pombe kali kwa wingi ila sasa ni mtu msafi huku akitaja siri ya ushindi. 

Mshindi huyo wa Oscars amepanga kusherekea miaka 10 ya utimamu wake kutoka katika dawa za kulevya katika siku yake ya kuzaliwa atakapotimiza umri wa miaka 70 mnamo Desemba mwaka huu. 

Huyu ni miongoni wa waigizaji waliofanikiwa sana duniani katika kizazi chake kutokana na umahiri wa kazi zake, mwaka 2020 Jarida la The New York Times lilimtaja kama muigizaji bora wa karne ya 2021. 

Alipata umaarufu pindi alipoigiza katika tamthili ya kimatibabu ya St. Elsewhere kati ya mwaka 1982 hadi 1988, pamoja na filamu ya kivita, A Soldier’s Story (1984), kisha mwaka 1989 kushinda tuzo mbili za Oscars.  

Denzel anayefanya vizuri sasa kupitia filamu, Gladiator II (2024), katika mahojiano na Jarida la Esquire mapema wiki hii amekiri kuwa matumizi yake ya zamani ya dawa za kulevya na pombe yameacha athari katika afya yake.

“Nimefanya uharibifu mwingi kwenye mwili wangu lakini sasa nimekuwa msafi, ebu tazama. Mambo yanafunguliwa kwangu sasa – kama kuwa na umri wa miaka 70,” alisema Denzel na kuongeza, 

“Ni kweli na ni sawa, kwa umri wa miaka 70 hii ni sura ya mwisho, ikiwa nitapata thelathini nyingine ya kuishi, unajua nataka kufanya nini? Mama yangu alifika miaka 97, kwa hiyo nitafanya yale bora niwezavyo,” alisema.

Denzel alifichua kuwa alijihusisha na aina mbalimbali za ulevi kwa miaka mingi lakini hatimaye mvinyo uligeuka kuwa msaada mkubwa wa kumtoa katika urahibu huo. 

“Sikuwahi kutosheka na sikuwahi kuchoshwa na pombe ila nilikuwa na wazo hili bora la kuonja mvinyo kama mbadala wa mambo hayo, hivyo ndivyo ilivyokuwa mwanzoni ingawa ni jambo gumu sana,” alisema.

Anasema alijifunza kunywa mvinyo kistaarabu akiwa na miaka 61 na ataendelea hadi atakapofikisha 82 maana nyumbani amebakiza chupa za Dola4,000 tu, na kwa muda wote amepata ladha bora na familia yake ilimpongeza kwa hatua hiyo. 

Denzel alianza utamaduni huo kwa kuagiza chupa mbili kutoka katika dula la Gil Turner’s Fine Wines & Spirits huko Hollywood, mke wake, Pauletta alimuuliza kwa nini anaagiza chupa mbili tu kila wakati. 

Alimjibu kwa sababu akiagiza zaidi, atakunywa zaidi, anaweza kunywa zote mbili wakati wa mchana tu. Hata hivyo, licha ya tabia yake hiyo, Denzel alisema alijizuia kunywa wakati akifanya kazi zake mbalimbali.

Ikumbukwe Juni 25, 1983 ndipo Denzel Washington walifunga ndoa na mkewe Pauletta Peason na tayari wamejaliwa kupata watoto wanne. Mwaka 1995 wawili hao walirudia viapo vyao vya ndoa nchini Afrika Kusini ambapo Desmond Tutu alihudhuria.