
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Tanzania, Charles Kichere amesema deni la Serikali limeongezeka kufikia Sh97.35 trilioni Juni 30, 2024 kutoka Sh82.25 trilioni kwa mwaka 2022/23.
Kwa mujibu wa CAG, deni hilo bado ni himilivu kutokana na viashiria vikuu alivyovitaja ikiwemo thamani halisi ya deni na pato la Taifa.
CAG ameyasema hayo leo Alhamisi, Machi 27, 2025 alipokuwa akisoma ripoti yake kuhusu mwenendo wa deni la Serikali wakati akikabidhi ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Mpaka kufikia Juni 30 2024 deni la Serikali lilifikia Sh97.35 trilioni, kiasi hiki kimeongezeka kutoka Sh82.25 trilioni likichoripotiwa mwaka wa fedha 2022/23 ni sawa na ongezeko la Sh15.1 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 18.36,” amesema.
Amesema deni hilo linajumuisha deni la ndani ambalo ni Sh31.95 trilioni na la nje la Sh65.40 trilioni.
CAG amesema tathmini la uendelevu wa deni la Serikali imebaini kuwa deni la Taifa bado ni himilivu.
“Viashiria vikuu vinaonyesha kuwa thamani halisi ya deni la nje ni asilimia 23.6 ya pato la Taifa chini ukomo wa asilimia 40, na deni la jumla ni asilimia 41.1 ya pato la taifa chini ya ukomo wa asilimia 55,” amesema.
Kwa mujibu wa Kichere, malipo ya deni kwa mapato ya mauzo ya nje ni asilimia 127.5 chini ukomo wa asilimia 180 na malipo ya deni kwa mapato ya serikali ni asilimia 14.5 chini ya ukomo wa asilimia 18.