De Bruyne ampa hofu Pep Guardiola

MANCHESTER, ENGLAND. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ametoa taarifa inayotia wasiwasi kuhusu utimamu wa kiungo wao, Kevin De Bruyne, baada ya staa huyo kuumia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Jumatano dhidi ya Inter Milan.

Licha ya kuanza vyema harakati za kulitetea taji lao la Ligi Kuu, Man City ililazimishwa suluhu na wababe hao wa Italia.

Mbali ya sare, Guardiola pia alipata pigo baada ya kulazimika kumtoa nje Kevin De Bruyne katika kipindi cha kwanza kutokana na jeraha ambalo linaripotiwa kuwa huenda likamweka nje kwa muda.

De Bruyne alionekana kuumia kabla ya kuamua kukaa chini mwenyewe huku ripoti zikieleza alikuwa amepata maumivu kwenye maeneo ya paja.

Baada ya kuumia, nafasi yake ilichukuliwa na Ilkay Gundogan ambaye aliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Baada ya mechi, Guardiola aliulizwa kuhusu hali ya fundi huyo na akasema: “Sijui, bado sijazungumza na madaktari. Nitakuwa na habari zaidi nitakapofanya mawasiliano na watalaamu. Tutamtathmini kesho na tutajua lakini naona hali siyo nzuri.”

Ikiwa De Bruyne atakaa nje kwa muda inaweza kuwa pigo kwa Man City inayokwenda kucheza na Arsenal wikiendi hii.

Mbali ya mchezo huo, ratiba inaonekana kuwa ngumu kwa Man City kwani watahitaji pia kucheza mechi mbili ndani ya siku tatu ambapo watapumzika siku moja tu baada ya kucheza na Arsenal kisha watavaana na Watford kwenye Carabao.