Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga (DC), Julius Mtatiro ametoa siku saba kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya chini kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuwasaka wanafunzi 26 ambao hawajaripoti kidato cha kwanza licha ya kuchaguliwa.
Hayo yamesemwa jana Jumatano, Februari 19, 2025 katika kikao kazi cha udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajaripoti, kilichofanyika katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM) kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
“Hawa watoto 26 ambao hawajaripoti kidato cha kwanza licha ya kufaulu na kuchaguliwa kujiunga natoa siku saba wasakwe watendaji, maofisa tarafa, walimu wakuu wa shule, waratibu elimu kata, watendaji wa kata kutoka halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,” amesema Mtatiro.

Baadhi ya wazazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameeleza sababu ambazo zinaweza kusababisha watoto hao kutoripoti shuleni.
“Baadhi ya wanafunzi hawajaripoti shuleni kwa sababu za ugumu wa maisha wanayoishi, unakuta mzazi hana fedha ya kumuhudumia mtoto mahitaji ya shule wakati mwingine hata mahitaji ya nyumbani pia wanakosa inakuwa ni ngumu kwa upande wake,” amesema Yohana John.
“Baadhi yetu wazazi hatujapanuka kiakili na kuwa na uelewa juu ya umuhimu wa elimu suala la kusoma hatuzingatii kinachozingatiwa ni uangalizi wa mifugo na mashamba hasa kwa maeneo ya vijijini,” amesema Salome Lushinge.
Mzazi mmoja kutoka kata ya Ngokolo, Monica Justine amempongeza mkuu wa wilaya kwa zoezi hilo la msako kwani litasaidia watoto wetu kupata elimu na kuepuka mimba na ndoa za utotoni.
“Zoezi hili litasaidia sana hasa kuepukana na mimba na ndoa za utotoni kwa sababu mda mwingi watoto hao watakuwa shuleni na pia elimu ni ufunguo wa maisha itawasaidia watoto kupata mwangaza wa maisha yao ya baadaye,” amesema Justine.
Mbali na hilo Mtatiro amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wazazi ambao watoto wao hawajaripoti huku akiwapongeza viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya chini kwa juhudi zilizofanywa hadi kiasi kikubwa cha wananfunzi kuripoti kidato cha kwanza.
“Tutawachukulia hatua kali wazazi na walezi wa watoto hao ili waripoti shule mara moja, mpaka tarehe ndani ya siku 7 wawe wameripoti shule watoto hao, nje na hapo nitaunda kikosi kazi mahili kitakachokwenda kuwarudisha watoto hao.

Haiwezekani Serikali itumie nguvu nyingi kujenga miundombinu mizuri, bora na rafiki kwa ajili ya watoto hao halafu mzazi au mlezi akatishe ndoto zao na mimi kama mkuu wa wilaya nitahakikisha kwa nguvu zangu zote suala hili nalishughulikia ipasavyo,” amesema Mtatiro.
Kwa upande mwingine, Mtatiro amewataka walimu wakuu kuwasimamia walimu katika suala la ufundishaji ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi huku akiutaka uongozi wa manispaa ya Shinyanga kuandaa siku ya kuwapongeza walimu na shule za Sekondari zilizofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne.
Hata hivyo, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa mwaka wa masomo 2025 jumla ya wanafunzi 4,274 wavulana wakiwa ni 1,867 na wasichana wakiwa 2,407 walichaguliwa kijiunga na masomo ya kidato cha kwanza.