DC awashukia viongozi wanaoweka siasa kwenye miradi ya kijamii

Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julias Mtatiro, amewaonya viongozi wa kiserikali wanaohusisha siasa katika miradi ya kijamii, hasa miradi ya kupeleka  maji vijijini.

Amesema kuingiza siasa kunakwamisha utekelezaji wa miradi hiyo na kusababisha kutokamilika kwa wakati.

Mtatiro amesema kuchelewa kwa miradi hiyo kunawaathiri wananchi, kwani wanakosa huduma muhimu ya maji kwa muda mrefu.

Mtatiro aliyasema hayo jana katika hafla fupi ya uwekaji saini mkataba wa kuanzisha mradi wa maji utakaotoka Ziwa Victoria na kuyapeleka katika kijiji cha Lyagiti kilichopo kata ya Lyabukande, wilayani Shinyanga.

“Huwa sipendi kusimamia miradi inayogharimu pesa nyingi kisha ianze kusuasua, na hii inasababishwa na siasa nyingi bila utekelezaji mzuri.

“Hali hii inawasababishia wananchi kuteseka kwa kipindi kirefu kwa sababu miradi haiwekewi kipaumbele na haikamiliki kwa wakati. Viongozi wa aina hii ni lazima wachukuliwe hatua,” amesema Mtatiro.

Pia, Mtatiro amewaasa wananchi kuachana na imani potofu ya kuwafuata wazee wao kwa kufuata yale waliyoyafanya, badala yake amewataka kuishi kulingana na mazingira ya sasa kwa kuvuta maji katika makazi yao.

“Msitake kuishi kama wazee wenu walivyoishi, kama hakuwa na maji nyumbani, huenda alifanya jambo ambalo huwezi kulifanya kwa sasa. Fanya kile unachoweza kwa wakati huu, kama kuchangamkia fursa na kuvuta maji katika makazi yetu,” alisema Mtatiro.

Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Shinyanga, Emael Nkopi, alisema kuwa mradi huo wa maji unagharimu Sh800 milioni.

Alisema mradi huo utatumia maji kutoka Ziwa Victoria na utahudumia wananchi 3,500.

“Kati ya vijiji 126 katika wilaya yetu, vijiji 75 vinapata maji kwa njia ya bomba, na vingine vinategemea maji ya kisima,” alisema Nkopi.

Mkandarasi wa mradi huo kutoka kampuni ya ujenzi Halem, Clemence Changu Katobesi alisema muda wa mradi huo ni mwaka mmoja na mtandao wake una urefu wa kilomita 16.

“Tutamaliza mradi kwa wakati bila kuwapo na ongezeko lolote la gharama, pia tunaomba ushirikiano na wananchi katika kulinda vifaa hivi vya ujenzi kuepuka hujuma ambazo zitarudisha nyuma mradi huu,” alisema Katobesi.

Diwani wa Kata ya Lyabukende, Luhende Kawiza, alisema kuwa mradi huu utawasaidia wananchi, hasa wanawake na wasichana, kwa kuokoa muda wao na kuwapa fursa ya kushughulika na shughuli nyingine za kijamii, badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.