DC aagiza waliohujumu miundombinu ya reli Moshi wasakwe

Moshi. Zaidi ya vifungio 95 vinavyoshikilia mataluma ya reli katika kipande cha miundombinu hiyo Moshi-Arusha, mkoani Kilimanjaro vimeibiwa na watu wasiojulikana.

Hali hiyo inahatarisha usalama wa watumiaji wa usafiri wa treni.

Tukio hilo lilitokea Aprili 21, mwaka huu ambapo inadaiwa watu hao waliong’oa vifungashio hivyo eneo la  Bondeni, Manispaa ya Moshi na kuondoka navyo.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kufanya msako na uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliofanya uharibifu huo.

“Tumepata taarifa za uharibifu wa miundombinu ya reli katika kipande chetu cha reli ya Moshi, tukio hili limetokea saa tano asubuhi jana, inaonekana kuna watu wasio waaminifu wameanza kufanya hujuma na uharibifu wa miundombinu hii ya reli,”amesema DC Mnzava.

Amesema, “wametoa pini reli zinazoshikilia mataluma takriban 90 hivi na kwa taarifa za awali inaonyesha ni wanaouza vyuma.”

Aidha mkuu huyo wa wilaya amesema wanaendelea kushughulikia changamoto hiyo iliyojitokeza ili shughuli za usafirishaji na usafiri ziweze kurejea.

“Tunaendelea kushughulikia changamoto hiyo kuhakikisha tunarejesha zile pini ili miundombinu ikae sawa ili huduma za usafiri ziendelee na treni iweze kupitia bila shida,”amesema DC Mnzava

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuitunza na kuilinda miundombinu hiyo na Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuiimarisha.

“Niwaombe wenzetu wa reli wawe wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika kipande chote cha reli hii hapa kwetu na kwingine kote ili kuhakikisha usalama unakuwepo wa kutosha wakati wote,”amesema DC Mnzava.

Mmoja wa wananchi wa eneo la kata ya Bondeni akionyesha moja ya vifungio vya reli ambavyo vimeng’olewa na kuibiwa, Manispaa ya Moshi.

Naye, Mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni, Abdallah Hussein, amesema baada ya kupata taarifa hizo walifanya eneo la tukio na kukuta miundombinu hiyo imeibiwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *