Dawasa yajitosa biashara saa 24 Kariakoo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) wameanza utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila la kutoa huduma saa 24 eneo la Kariakoo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha biashara kwenye eneo hilo haziathiriwi na taasisi zingine zinazotoa huduma za kijamii ikiwamo Dawasa.

Februari 27, 2025 katika kilele cha uzinduzi wa biashara saa 24 eneo la Kariakoo, Chalamila alisema Serikali imejipanga kuhakikisha biashara zifanyike usiku kwa ufanisi.

“Dhana ya kufanya biashara saa 24 eneo la Kariakoo haihusu biashara pekee bali hata taasisi za umma zinazohusika moja kwa moja na jamii nao wanatakiwa kuwepo eneo hili na kutoa huduma saa 24 kama ilivyo kwa wafanyabiashara,” alisema Chalamila.

Kutokana na hilo, usiku wa kuamkia leo Jumapili, Machi 2, 2025, watumishi wa Dawasa wamefanya uzibuaji wa mifereji maeneo ya Kariakoo.

Dawasa wameanza kuchukua hatua hiyo baada ya uwepo wa mifereji yenye kutiririsha majitaka maeneo mbalimbali ya eneo hilo hivyo kusababisha kero kwa wafanyabiashara.

Mkurugenzi wa huduma za usafi wa mazingira Dawasa, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema mamlaka inachagiza nia ya Serikali ya awamu ya sita ya kufanya biashara saa 24 kwa kuhakikisha uwepo wa watoa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.

Pia, amesema kutakuwepo vifaa vya kisasa vya uzibuaji na usafishaji wa mifereji ya majitaka vitakavyosaidia kuweka eneo la Kariakoo safi muda wote.

“Tumejipanga kuhudumia wafanyabiashara na wageni wanaokuja kupata huduma katika eneo hili la Kariakoo kwa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kisasa vya kuweza kuzibua na kusafisha line kubwa za majitaka zinazoanzia inchi sita  hadi 24.

“Pamoja na kufungua mabwawa ya majitaka Vingunguti na Kurasini kuanza kufanya kazi saa 24 kwa ajili ya kupokea magari yaajitaka,” amesema Mhandisi Ndibalema.