
Dar es Salaam. Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) Mhandisi Mkama Bwire amesema sababu kubwa ya kukosekana kwa maji kwenye jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani ni kuharibika kwa mtambo wa Ruvu juu.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam na mkoa wa Pwani leo Machi 7, 2025 makao makuu ya Dawasa zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Kwa jiji letu la Dar es Salaam linategemea kupata maji kutoka chanzo chetu cha mto Ruvu ambapo tumefunga mitambo Ruvu juu na Ruvu chini, lakini kwa wiki moja iliyopita mtambo wa Ruvu juu ulipata matatizo ndio sababu ya maeneo mengi kukosa maji,” amesema Bwire.
Kauli ya Bwire imekuja kukiwa na malalamiko ya wananchi kwenye baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam kukosa huduma ya maji.
Ameendelea kwa kusema ni kawaida mtambo wa maji kuharibika na ikitokea hivyo ndio sababu ya uzalishaji wa maji kupungua, huku akisema tayari Serikali imeshaagiza mitambo mipya ikitarajia kufika nchini na kuanza kazi Julai mwaka huu.
Aidha amesema mtambo wa Ruvu juu unahudumia maeneo mengi yakiwemo Kinyerezi, Makabe, Machimbo, Tabata, Temeke, Ubungo, Kimara na Mbezi.
Endelea kufuatilia katika mitandao ya Mwananchi