Davido ampa maua yake D’banj

Nigeria, Mwimbaji wa Nigeria, Davido (31) amemshukuru mwanamuziki mwenzake, D’banj (44) kwa kusema wimbo wake, Oliver Twist (2012) ndiyo uliwafungulia milango ya kimataifa wasanii wa nchi hiyo na hata kubadili mtazamo wake kuhusu muziki wa Afrika.

Mnamo Juni 2011 D’banj alisainiwa na lebo ya Kanye West, Good Music na kutoa wimbo huo wenye mahadhi ya EDM na Afrobeats ambao ulitikisa sana hadi staa wa Bongofleva, Linah aliurudia (refix) kwa namna yake.

Wimbo huo uliokuwa wa kwanza kutoka katika albamu ya mkusanyiko ya DB Records, D’Kings Men (2013) ulishinda tuzo ya The Headies pamoja na tuzo mbili za Channel O huku ukishika namba mbili chati ya R&B nchini Uingereza.

D’banj ambaye alishirikiana na Don Jazzy kuanzisha lebo ya Mo’Hits, pia ameshinda tuzo za MTV Europe 2007, MTV Africa 2009 na BET 2011.

Na Agosti 2013, video ya wimbo ‘Oliver Twist’ ilifikisha ‘views’ zaidi ya milioni 21.5 YouTube na kuandika rekodi kama video ya kwanza ya muziki nchini Nigeria iliyotazamwa zaidi katika mtandao huo.

Akizungumza na Apple Music, Davido amesema baada ya kushuhudia mafanikio ya wimbo huo wa D’banj ‘Oliver Twist’ alipata hamasa ya kuzingatia muziki wa Kiafrika pamoja na kukumbatia urithi wake wa kitamaduni

“Kwa D’banj ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona msanii wa Nigeria akiushika ulimwengu, hakuna mtu Marekani aliyekuwa akiwapa nafasi ya wasanii wa Nigeria katika maonesho, ila hiyo ilibadilika nilipomuona Kanye West kwenye video ya Oliver Twist,” alisema.

“Baada ya mafanikio ya Oliver Twist, Wamarekani walianza kuwapa nafasi kina D’banj, 2Face, P-Square na wasanii wengine wa Afrika katika maonesho yao na kuwalipa takribani Dola1 milioni kwa kila onyesho,” alisema Davido.

Utakumbuka Davido alianza muziki katika kundi la KB International nchini Marekani, alipata umaarufu alipoachia wimbo wake, Dami Duro (2011) ambao ni wa pili kutoka kwa albamu yake ya kwanza, Omo Baba Olowo.

“Kwa hiyo kufuatia kuvuma kwa Oliver Twist niliamua kubadilika na kuanza kufanya muziki wa Kiafrika kwa sababu huko ndiko ninapotokea,” alisema Davido ambaye alizaliwa Atlanta, Marekani na kukulia Lagos, Nigeria.

Ukubwa wa Davido Afrika uliongezeka baada ya mwaka 2016 kusaini mkataba na lebo ya Sony Music, kisha miezi michache baadaye kuanzisha lebo yake, Davido Music Worldwide (DMW) na kuwasaini Dremo na Mayorkun.

Mwaka uliofuatia alirekebisha mkataba wake na Sony Music na kutoa nyimbo tano zikiwemo ‘If’ na ‘Fall’ ambao ulikuwa wimbo wa kwanza Nigeria kukaa kwa muda mrefu zaidi chati za Billboard na hadi sasa ndio wimbo wa Davido uliotazamwa zaidi YouTube ukiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 291.