Dar Swim kushiriki mashindano ya taifa Kenya

TIMU ya kuogelea ya Dar Swim Club inatarajia kushiriki mashindano ya taifa ya Kenya ‘Kenya Aquatics Long Cource Championship’ yanayotarajiwa kuanza Jumamosi, Februari 15 hadi 16.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Kanisi Mabena amesema wameondoka nchini leo ‘jana’ na waogeleaji sita anaoamini wataenda kufanya vizuri kwenye mashindano hayo kutokana na walivyofanya maandalizi ya kutosha.

“Nafasi tuliyoipata kwa kushiriki mashindano hayo nina imani kubwa kuwa ni fursa nzuri kwa waogeleaji kutumia mashindano hayo kwa lengo la kuongeza uzoefu,” amesema na kuongeza;

“Kwenye mashindano hayo Tanzania inatarajiwa kuwakilishwa na timu tatu moja wapo ni timu yangu, Riptide ya jijini Arusha na Tanzania Dwim Squad itakayojumuisha waogeleaji kutoka timu kadhaa.”

Alisema kigezo cha kupata mwaliko kwenye mashindano hayo waogeleaji wamewekewa muda ambao wanatakiwa kuufikia na timu yake imekidhi hivyo vigezo ndiyo maana imechaguliwa.

“Wachezaji sita ambao nimewabeba kwenye timu yangu wamekidhi vigezo na matarajio ni kwenda kuvunja rekodi zao ili kufuzu mashindano yanayotarajia kufanyika Afrika Kusini pamoja na kutwaa medali,” amesema na kuongeza;

“Wachezaji ambao wanatarajia kuanza ushindani wa kuogelea Jumamosi ni Blake Williams, Camilla Kyenekiki, Austin Durr, Jackson Durr, Samantha Moshi na Oscar Liebchen.”