Dar Sprint yamtega tena Birdi Tanganyika Packers

BAADA ya kushinda mashindano matatu mfululuzo ya mbio za magari hadi nusu ya mwaka huu, Manveer Birdi atakuwa na mtihani mwingine mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Tanganyika Packers kuthibitisha ubora wake nyuma ya usukani.

Toyota Dar Sprint, mbio fupi za mzunguko, ndiyo mtihani ambao Birdi anatakiwa kuushinda na kuudhihirisha umma kuwa yeye ndiye mbabe wa vita ya injini nchini Tanzania.

Mashindano haya ya siku mmoja, ni raundi ya tatu ya ubingwa wa mbio fupi jijini Dar es Salaam na Birdi ameshinda raundi zote mbili za awali kwa kishindo kikubwa.

Birdi anaingia viwanja vya Tanganyika Packers siku saba baada ya kushinda mbio za magari za Mkwawa, ambazo ni raundi ya kwanza ya ubingwa wa magari kitaifa (National Rally Championship) kwa mwaka huu akiwa pia ni bingwa mtetezi  baada ya kuibuka mshindi wa jumla wa mwaka 2024.

Kwa mujibu wa waandaaji, chama kinachosimamia mchezo wa mbio za magari nchini (AAT), zaidi ya washiriki 50 wanategemewa kushiriki katika mashindano ya mwishoni mwa juma.

Kwa mujibu wa AAT, idadi hiyo inahusisha madereva wa magari maalum ya mashindano (homologated rally cars) magari ya kawaida (ordinary cars) pamoja pikipiki za gurudumu nne (quadbikes).

“Madereva nyota, akiwamo, Manveer Birdi ambaye ni bingwa wa taifa wa mbio za magari mwaka 2024 na pia bingwa mtetezi wa mashindano haya, ni mmoja wa washiriki na kuwepo kwake kutazidisha ushindani katika mchezo,” ilisema AAT katika taarifa kwa waandishi wa habari.

Mbio fupi za Toyota Dar Sprint zinakuja tena Tanganyika Packers takriban miezi mitatu baada ya baada ya kufanyika kwa mbio za magari za Usiku wa Mbalamwezi (Moonlight Rally) ambazo mshindi wake alikuwa alikuwa Manveer Birdi akifuatiwa na Randeep Singh katika nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa AAT, wote walioshiriki raundi mbili za awali watakuwapo tena safari hii, na wengi wao wakipania kuuangusha ufalme wa Birdi.

Mmoja wa madereva wanaowania kuupoka ufalme wa Birdi ni pamoja na bingwa wa zamani, Dharam Pandya ambaye amerudi rasmi mchezoni mwaka huu.

Wapinzani wengine ni Harinder Deere, Irfan Aladin, Zubair Piredina, Salim Haji, Ethan Taylor, Kelvin Taylor na David Bicco.

“Tunawakaribisha wapenzi na mashabiki wa mbio za magari kufika kwa wingi kwenye viwanja vya Tanganyika Packers ili kujua nani ni bingwa wa raundi hii,” alisema mwenyekiti wa kamisheni ya mbio za magari nchini, Satinder Birdi.

Katika mashindano yaliyopita, Birdi aliwaonyesha mabingwa wa zamani kuwa yeye ndiye kinara wa kweli wa mchezo baada ya kushinda mbio fupi za Dar Rally akitumia muda wa dakika 1 sekunde 43 na nukta 77 na kumaliza mbele ya Randeep Birdi aliyetumia muda wa dakika 1, sekunde 44 na nukta 49 akiendesha gari ya Mitsubishi Evo 9.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *