Dar, Pwani na Zanzibar kukosa umeme kwa siku sita

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha changamoto za usambazaji wa huduma ya nishati ya umeme kwa wananchi, inafanyika kwa ufanisi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuboresha miundombinu yake kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani.

Kutokana na hatua hiyo, baadhi ya maeneo katika Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani yatakabiliwa na changamoto ya huduma ya umeme kwa siku sita mfululizo kwa nyakati tofauti kwenye baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tanesco kwa vyombo vya habari leo Jumatano, Februari 19, 2025 hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya kufanyika kwa maboresho kwenye kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Msongo wa Kilovoti 220 kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam.

Katika maboresho hayo, Tanesco litafunga mashineumba (Transformer) mpya kubwa yenye uwezo wa MVA 300 ili kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo husika ikiwa ni mkakati wa kumaliza tatizo la kuzidiwa kwa mashine hiyo kutokana na ongezeko la watumiaji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maboresho hayo yataanza Jumamosi ya Februari 22 hadi 28, 2025.

“Hatua hii ni muhimu kwa Shirika katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake kutokana na ongezeko la wateja. Ongezeko hilo limesababisha kituo kuzidiwa hivyo, tutafunga mashineumba mpya yenye uwezo wa MVA 300 ili kumaliza changamoto hiyo,” imesema taarifa hiyo kutoka Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Umma.

Kutokana na hali hiyo, Tanesco imewaomba radhi wateja wake watakaokabiliwa na changamoto hiyo huku likiahidi kukamilisha kazi kwa wakati ili huduma zirejee kama kawaida.