Dar kinara watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani

Dodoma. Mkoa wa Dar es salaam umetajwa kuwa kinara kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ikifuatiwa na mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha na Iringa huku mikoa inayoongoza kuchangia maeneo ya miji kuwa na watoto zaidi ni Kagera, Geita, Kigoma, Dodoma, Mwanza na Shinyanga.

Aidha katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 jumla ya watoto 8,372 wanaoishi na kufanya kazi mtaani waliokolewa na kupatiwa huduma mbalimbali ambapo 1,056 kati ya hao wapo katika makao ya watoto na nyumba salama, 86 wako kwa walezi wa kuaminika na waliobakia waliunganishwa na familia zao.

Watoto 1,346 kati ya waliookolewa walipatiwa vifaa vya shule na mahitaji mbalimbali huku 43 kati yao waliunganishwa na vyuo vya ufundi ambapo 27 wamehitimu na wawili wanafanya kazi za kujitolea katika makazi ya wazee.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Aprili 9, 2025 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea siku ya mtoto anayeishi na kufanya kazi mtaani, jijini Dodoma.

Dk Gwajima amesema maadhimisho hayo yatafanyika Aprili 12, 2025 kwa kila mkoa na kitaifa yatafanyika mkoani Mtwara.

“Aidha, mikoa inayoongoza kuwa na watoto wengi wanaoishi na kufanya kazi mtaani ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha na Iringa huku mikoa inayoongoza kuchangia maeneo ya miji kuwa na watoto zaidi ni Kagera, Geita, Kigoma, Dodoma, Mwanza na Shinyanga,” amesema Dk Gwajima.

Amesema ili kuhakikisha watoto wote wa Tanzania wanastawi katika mazingira rafiki na salama ya malezi, makuzi na maendeleo yao, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.

Ametaja hatua hizo kuwa ni kushughulikia migogoro ya ndoa ambapo jumla ya migogoro 16,095 imeshughulikiwa kupitia ofisi za ustawi wa jamii nchi nzima katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Machi, 2025 ambapo, mashauri 2,555 kati ya hayo yamepelekwa mahakamani na 10,423 yamesuluhishwa na mengine yanaendelea kusikilizwa.

“Kushughulikiwa kwa migogoro hii kunasaidia kupunguza wimbi la watoto kuingia mtaani,” amesema Dk Gwajima.

Amesema hatua nyingine ni kufanya uratibu wa huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024 jumla ya manusura 27,479 walipatikana na kati yao kulikuwa na  watoto 15,040 na watu wazima 12,439.  Walipata huduma katika madawati ya jinsia na watoto ya Jeshi la Polisi na wengine wamehudumiwa na maofisa ustawi wa jamii katika halmashauri zote.

Dk Gwajima amesema huduma ya matunzo na malezi kwa watoto imeendelea kutolewa kwenye makao mawili ya watoto yanayomilikiwa na kuendeshwa na Serikali yenye jumla ya watoto 253 yaliyopo Kikombo (Dodoma) na Kurasini (Dar es salaam) ambapo watoto hupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo elimu, afya, elimu ya kiroho na msaada wa kisaikolojia.

“Vilevile, kuna makao binafsi 388 yenye watoto 14,215  yanayotoa huduma za msingi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi ambao, wana changamoto kwenye familia ili kuhifadhiwa kwa muda wakati changamoto zao zinashughulikiwa,” amesema Dk Gwajima.

Amesema Serikali imeanzisha madawati 14 katika vituo vya usafiri ambapo maofisa ustawi wa jamii hutoa huduma kwa watoto na makundi maalumu, lengo ni kudhibiti watoto wenye viashiria vya kuingia mtaani.

Amesema madawati haya yapo katika mikoa 11 ambayo ni Tabora, Mbeya, Dodoma, Kagera, Arusha, Morogoro, Songea, Shinyanga, Njombe, Mwanza na Dar-es-Salaam

Dk Gwajima amesema Serikali inaendelea kuhudumia kaya zenye watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ambapo kwa kipindi cha Julai 2024 mpaka Machi 2025 jumla ya kaya 43,563 zimewezeshwa na kuimarishwa kiuchumi kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ya biashara na ujuzi.

“Kwa sasa Serikali itajikita zaidi kwenye mikakati ya kuziba mianya inayosababisha watoto kwenda kuishi mtaani kupitia modeli ya kitaalamu ya “Close the Tap” kwa kushughulikia changamoto za kifamilia na kiuchumi zinazowasukuma kuingia mtaani.

“Hivyo, tunapojiandaa kuadhimisha siku hii, kwa kuanzia, Serikali imeandaa matukio ya kuelimisha jamii juu ya tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *