
Lagos, Nigeria. Tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote raia wa Nigeria amefichua kuwa anajutia uamuzi wake wa kutoinunua Klabu ya Arsenal ya England wakati thamani yake ilikuwa, badala yake ameamua kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa kiwanda cha kusafisha mafuta kilichopo Nigeria.
Kwa sasa, Arsenal inamilikiwa na bilionea wa Marekani, Stan Kroenke na hakuna dalili kwamba yuko tayari kuuza klabu hiyo kutokana na mafanikio ambayo imekuwa ikiyapata kila siku.
Mwaka 2019, Dangote alionyesha nia ya kuinunua Arsenal lakini aliamua kuwekeze kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta nchini kwao ambacho kingempa faida kubwa zaidi kutokana na uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 kwa siku.
Kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya hivi karibuni, Dangote ambaye amewahi kukiri mara kwa mara kuwa ni shabiki wa Arsenal, amesema alipanga kumaliza mradi wake wa mafuta ndipo arudi kununua klabu hiyo, lakini anajuta kwani thamani ya Arsenal imekuwa kubwa kuliko wakati ule kutokana na kufanya vizuri.
“Nilikuwa naweza kuinunua Arsenal kwa dola 2 bilioni lakini nisingeweza kumalizia mradi wangu mkubwa nchini Nigeria, ilikuwa ni aidha kumalizia mradi au kununua klabu, ingawa najutia uamuzi wangu.
“Kwa sasa sidhani kama nina fedha za ziada za kununua klabu hii tena kwa kuwa thamani yake pia imepanda sana hadi dola bilioni 4 (zaidi ya 10 trilioni), nitaendelea kuwa shabiki mkubwa wa Arsenal.
“Kila siku nimekuwa nikiangalia mechi za Arsenal na nitaendelea kufanya hivyo kila wakati lakini suala la kuinunua kwa sasa haliwezekani,” alisema bilionea huyo akizungumza na Bloomberg.
Licha ya majuto yake, Dangote anasimama na uamuzi wake wa kuwekeza kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta, ambacho kinatarajiwa kupunguza utegemezi wa Nigeria kwenye mafuta na kumaliza ruzuku ya mafuta inayogharimu taifa hilo mabilioni ya fedha kila mwaka.
Arsenal inatajwa kama moja ya klabu kubwa kwenye soka la England ikiwa imetwaa ubingwa wa ligi hiyo mara 13, Kombe la FA mara 14, imetwaa ngao ya Jamii mara 17. Kwa sasa ikiwa chini ya kocha Mikel Arteta inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa pia kwenye michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.