Dalali: Sarungi aliwasaidia Simba, Yanga

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali amesema mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani marehemu Profesa Philemon Sarungi alikuwa msaada mkubwa kwa wanasoka nchini wakiwemo wa timu za Simba, Yanga na Taifa Stars.

Sarungi (89) ambaye ni Waziri wa zamani na mbunge wa Rorya, mkoani Mara alifariki dunia jana Jumatano Machi 5, 2025 saa kumi jioni nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Sarungi ambaye tangu mwaka 1990 hadi 1992, alikuwa Waziri wa Afya, na shabiki mkubwa wa Simba alikuwa msaada kwa kuwatibia wachezaji ambao walikuwa wanasumbuliwa na changamoto ya mifupa kama anavyoeleza Dalali  ambaye alifanya naye kazi kwa muda mrefu.

“Sarungi kuanzia mwaka 1996 hadi 2005, alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Walezi Simba alikuwa anatatua migogoro mbalimbali ndio maana mwaka 2006 aliteua kamati ya muda ya kuiongoza Simba ambapo Michael Wambura alishika nafasi ya uenyekiti na mimi nikawa mjumbe,” alisema Dalali na kuongeza;

“Baada ya uongozi wa mpito kudumu kwa mwaka mmoja ndipo nikaingia madarakani kuanzia 2007 hadi 2010, nilishuhudia akiwasaidia wachezaji wa Simba, Yanga na Stars katika matibabu ya mifupa tena kwa kujitolea, hivyo anakumbukwa kwa hekima na utu wake.”

Dalali alisema Sarungi alikuwa mtu muhimu sana kwenye maendeleo ya soka nchini ndiyo maana baada ya kusikia taarifa za kifo chake, alikumbuka mambo mengi aliyoyafanya yatakayobakia kama alama ya kuheshimika ndani na nje ya Simba.