
MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Hassan Dalali amesema licha ya kuipa nafasi Simba ya kushinda mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao Yanga, Machi 8, lakini haijawahi kuwa rahisi tangu zilipoanza kuchezwa mwaka 1965.
Dalali alisema mchezo huo umejaa hisia ndiyo maana kuna watu wanakufa, wanaumia na kupata changamoto mbalimbali inapotokea timu anayoshabikia imepata matokeo tofauti na matarajio yake.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa timu yake, Simba, tangu Fadlu alivyoanza kuinoa, imekuwa na mabadiliko ya kiushindani na anaona ari ya wachezaji kujituma, jambo linalomwaminisha ina nafasi kubwa ya kuvuna pointi tatu.
Alisema kwa namna Fadlu alivyoijenga timu hiyo, anaamini mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Wanamsimbazi wanakwenda kushinda.
“Kiuhalisia haijawahi kutokea dabi rahisi, zinapokutana Simba na Yanga ni mechi iliyojaa hisia, ndiyo maana kuna watu wanakufa, wanaumia na kupata changamoto mbalimbali inapotokea timu anayoshabikia imepata matokeo tofauti na matarajio yake,” alisema Dalali na kuongeza.
“Nakumbuka mwaka 1975 kuna shabiki alikuwa anaitwa Marenda, alikuwa mkazi wa Mwanza, tulifungwa na Yanga mabao 2-1 mechi ilichezwa Zanzibar, hakukubaliana na matokeo, akajitosa katika kisima cha moto akafariki kifo kibaya sana, ni tukio ambalo sijawahi kulisahau katika maisha yangu.
“Ndio maana wachezaji na waamuzi wanapaswa kufahamu madhara yanayoweza kutokea pindi wakifanya kazi yao kwa kukosa uaminifu.”
Alisimulia tukio ambalo lilikuwa la kumfurahisha la dabi ya 2008 na Yanga ilipotea njia ikajikuta ipo Kimbiji na Simba ikapewa ushindi wa mezani.
“Ilikuwa mechi ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati, watu walijaa uwanjani, nikampigia simu marehemu Imani Madega kumuuliza mpo wapi mbona hamtokei uwanjani, akaniambia tumepotea tupo Kimbiji basi tukapewa ushindi wa mezani, maana timu yao haikufika muda unaotakiwa,” alisema Dalali ambaye aliiongoza Simba kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 ndipo akampisha Ismail Aden Rage.