
Arusha. Wanawake wameshauriwa kutumia vidonge vya vitamini ya foliki asidi kwenye lishe kabla na baada ya ujauzito ili kupunguza hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo, ikiwemo ya moyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Naiz Majani, amesema hayo leo Jumatatu, Machi 3, 2025 wakati akizungumza katika wiki ya wanawake inayoendelea jijini humo kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani Machi 8.
Amesema ni muhimu kwa mwanamke kutumia vidonge hivyo vya virutubisho vya foliki asidi kabla hajabeba mimba na ndani ya miezi mitatu ya mwanzo ili kupunguza hatari ya mtoto kuzaliwa na changamoto, ikiwemo ya moyo.
Aidha, Amesema visababishi vingine vya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo vinatajwa kuwa ni pamoja na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na vinasaba.
Amesema kwa sasa wanaendelea na kampeni maalumu ya kugundua matatizo ya moyo ya watoto wakiwa tumboni, kwani magonjwa ya moyo ya watoto yanapaswa kugunduliwa mapema ili yapatiwe matibabu sahihi.
Amesema tangu mwaka 2016 hapa nchini walipoanza kipimo cha Echocardiography, kinachofanyika mtoto akiwa tumboni, wamebaini changamoto kubwa wanayoiona ni kwamba watoto hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa.
Dk Majani amesema sababu za watoto kuzaliwa na matatizo ya moyo ni nyingi, lakini matatizo mengine yanatokea wakati mama akiwa mjamzito, ikiwemo kutokula vyakula bora vyenye virutubisho.
“Ndiyo maana tunawauliza kinamama hapa, umetumia foliki asidi ambayo inapaswa kutumika kabla mimba haijatungwa na ndani ya miezi mitatu ya kwanza?
“Kwa hapa Arusha, tumegundua wamama wengi wanachelewa kunywa foliki asidi. Wengi wanakunywa mimba ikiwa na mwezi mmoja, wengine miezi minne.
“Kingine kinachoweza kusababisha matatizo ya moyo kwa mtoto ni vinasaba, ndiyo maana tunasema kama una ndugu au ulishawahi kuzaa mtoto mwenye matatizo ya moyo, unaweza kupata mtoto mwenye tatizo. Aje apime mapema,” ameongeza.
Dk Majani amesema katika upimaji huo maalumu, unaohusisha makundi yote lakini zaidi wajawazito, tangu shughuli hiyo ianze Machi mosi, 2025, hadi leo wamewahudumia kina mama 91, na kati yao wajawazito ni 25.
“Kati ya hao wajawazito, wawili tumegundua watoto wao wana matatizo ya moyo. Tumeshawaandikia barua za rufaa kwenda hospitali watakazojifungulia, tumechukua taarifa zao muhimu, makadirio ya tarehe zao za kujifungua, na tutaendelea kuwafuatilia. Wakijifungua, wataletwa JKCI kuanza matibabu.
“Kwa upande wa watoto, hadi sasa tumewaona 25, na kati yao wawili tumewakuta wana matatizo ya moyo na wamepata rufaa kwenda JKCI kuanza matibabu. Tunaamini kampeni hii ikisambaa itasaidia watoto waliozaliwa kupatiwa matibabu mapema.”
Dk Majani amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha, hasa wajawazito, kuanzia wiki ya 20 ya ujauzito wakapime ili kujihakikishia usalama wa afya za watoto wao.
Pia amewashauri wazazi ambao wameshajifungua, lakini wanaona watoto wao hawakui vizuri au hawanyonyi vizuri wakapimwe.
Mmoja wa wajawazito aliyejitokeza katika kampeni hiyo maalumu ya kupima moyo wa watoto walioko tumboni, Mariam Juma, mkazi wa Muriet, ameshukuru kupata fursa hiyo ya kuangalia iwapo mtoto wake ana changamoto yoyote.
“Tunashukuru sana kwa elimu na upimaji huu. Awali, sikujua kuhusu hili suala, ila baada ya kusikia nimekuja, na namshukuru Mungu nimepimwa, nimekutwa mtoto wangu yuko salama, hana tatizo, na nina uhakika wa kujifungua mtoto asiye na changamoto ya moyo,” amesema.
Naye Prince Kimaro (24), amesema amekwenda kupima ili kujua kama ana tatizo lolote la moyo, kwani amekuwa akipata changamoto kadhaa.
“Kwa kipindi cha miezi minne, nimekuwa nikipata tatizo la mapigo ya moyo kwenda mbio. Nilienda hospitali hapa Arusha, nikapewa dawa na nimemaliza.
“Leo nimekuja kupima, wameangalia, sina tatizo, lakini nasubiri kipimo kingine waniangalie umeme wa moyo,”amesema na kuongeza;
“Nawasihi vijana wenzangu tujali na kuangalia afya zetu, kwani ndiyo mtaji wetu. Ukiwa huna afya nzuri, hata kazi hutaweza kufanya. Nilikuwa na shida kidogo, nikaona nije kutumia hii fursa kuangalia zaidi, nijue nasumbuliwa na nini na nipate matibabu sahihi,” amesema.