
Yanga imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Al Hilal kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mabao ya Adama Coulibaly dakika ya 63 na Yasir Mozamil (dk 90) yaliitibulia Yanga ambayo haikuwa imeruhusu idadi hiyo ya mabao tangu irejee katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita baada ya takribani miaka 25.
Mabao hayo yalitokea kutokana na safu ya ulinzi ya Yanga chini ya mabeki wa kati, Ibrahim Bacca na Dickson Job kutokuwa makini kuwazuia nyota wa Al Hilal ambao walionekana kuwa mafundi sana kwenye mipira ya kushtukiza.
Lakini pia washambuliaji wa Yanga walionyesha kiwango cha chini kwenye mchezo huo, huku wakikosa nafasi kadhaa za wazi ambazo zingeweza kubadili matokeo hayo.
Hata hivyo, msimu huu Yanga ilianza vizuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo hatua za awali hadi inafuzu makundi ilifunga mabao 17 bila ya nyavu zake kutikiswa, lakini michezo ya hivi karibuni imekuwa mibaya kwake.
Novemba 15 mwaka huu, Yanga ilifanya mabadiliko ya benchi la ufundi ikimuondoa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi na msaidizi wake Moussa N’Daw, nafasi zao zikachukuliwa na Sead Ramovic na Mustapha Kodro.
Leo ndiyo kimekuwa kibarua cha kwanza kwa makocha hao ambao wameanza kwa kichapo cha aibu kilichoibua maswali mengi, huku timu hiyo ya Jangwani ikicheza mechi tatu bila kupata ushindi.
Katika dakika 45 za kwanza za mchezo huo wa Kundi A, Yanga ilionekana kuanza kwa kasi huku Al Hilal ikiwa taratibu lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda mambo yalikuwa yakibadilika.
Prince Dube ambaye jana alikabidhiwa mechi hiyo maalumu ikipewa jina lake, alipata nafasi nyingi za kufunga lakini umakini mdogo ukaikosesha timu yake mabao.
Dakika hizo 45 za kwanza, Dube alikosa nafasi tatu za wazi ambao kama angekuwa makini basi angeifungia timu yake.
Kukosa kwa nafasi hizo kumeendelea kuibua maswali ambapo Dube msimu huu amekuwa hana wakati mzuri kitakwimu ukiachana na mabao matatu aliyofunga hatua ya awali katika michuano hiyo, hana bao lingine.
Bado kocha Ramovic atakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha wachezaji wake wanashika falsafa zake akitaka kuona timu inacheza soka la kasi lakini mbele kwenye umaliziaji baada ya jana kuonekana kuwa taratibu sana.
Mbali na Dube kukosa nafasi hizo, lakini kukosekana kwa Khalid Aucho eneo la kiungo mkabaji imeonekana kuitesa zaidi Yanga ambapo iliamua kumtumia Mudathir Yahya aliyesaidiana na Duke Abuya ambao muda mwingine walishindwa kuwamudu viungo wa Hilal.
Nguvu kubwa waliyokuwa nayo Al Hilal ilikuwa kutumia pembeni kufanya mashambulizi yake hasa upande wao wa kulia ambapo Steven Ebuela alionekana kumsumbua beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage.
Hata bao la kwanza lililofungwa na Coulibaly alitumia udhaifu wa upande huo wa Yanga lakini pia lile la pili lilipitia upande wa kulia wa Yanga.
Kwa ujumla, wachezaji wa Yanga katika mchezo wa jana walicheza kwa morali ya chini iliyowafanya kupoteza mchezo huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo mbele ya Al Hilal.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 16, 2022 katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa nchini Sudan na wenyeji Al Hilal kushinda 1-0. Kabla ya hapo, Oktoba 8, 2022 jijini Dar es Salaam, matokeo yalikuwa sare ya 1-1.
Ushindi huo unamfanya Kocha Florent Ibenge wa Hilal kuendelea kufurahia kukutana na Yanga kwani hajawahi kupoteza dhidi yao akishinda mara mbili nyumbani na ugenini na kutoa sare mara moja katika mechi tatu walizokutana.
Sikia makocha
Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge amesema: “Yanga ni timu kubwa, tulichokifanya ni kucheza kwa tahadhari, kipindi cha kwanza hakutuwa na mikakati ya ushindi, lakini kipindi cha pili ndiyo tulihitaji ushindi.
“Mpango huo ulikuwa ni kuhakikisha tunashambulia huku tukilinda lango letu kwa tahadhari kubwa baada ya kuona kipindi cha kwanza wapinzani wameshindwa kutufunga.”
Kocha Ramovic amesema: “Inaumiza, nimeanza na matokeo mabaya ya kipigo, kama timu kubwa tunarudi kujipanga na mechi zijazo, tunajua tuna mechi nyingi mbele, tutahakikisha tunafanya vizuri, kwa kuanza ni lazima tushinde mchezo wa ligi wa Jumamosi ijayo.”
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, TP Mazembe ikiwa nyumbani ilitoka suluhu dhidi ya MC Algier.