Dakika 90 za mtego kwa Taifa Stars

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars inakabiliwa na mechi ngumu ya ugenini dhidi ya Morocco kuanzia saa 6:30 usiku wa kuamkia kesho Jumatano ambao ni wa Kundi E kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Manispaa jijini Oujda nchini Morocco ambao unaingiza mashabiki 19,000 na utachezeshwa na refa Alhadi Mahamat kutoka Chad.

Ushindi katika mechi hii utaifanya Taifa Stars ifikishe pointi tisa na hivyo inaweza kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi lake.

Hapo Taifa Stars itaweka hai ndoto zake za kufuzu kwa mara ya kwanza kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kushindwa kufanya hivyo nyakati zilizopita kuanzia kombe hilo lilipoanzishwa.

Lakini kama Taifa Stars itapoteza mechi hiyo ya leo, maana yake Morocco itakuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwani itafikisha pointi 12 ambazo hazitofikiwa na timu za Tanzania, Niger na Zambia hata kama zikipata ushindi katika mechi zao za mwishoni kutokea kundi hilo.

Hata hivyo, hilo la Morocco litatimia iwapo Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) litaendeleza adhabu ya kuifungia Congo ambayo ni miongoni mwa timu zinazounda kundi hilo.

Taifa Stars inaingia katika mechi hii ikiwa haina kumbukumbu nzuri na wenyeji Morocco ambao mechi ya mwisho kuzikutanisha timu hizo, Tanzania ilipoteza kwa kichapo cha mabao 3-0.

Mbali na Morocco kufuzu, kichapo cha leo kitazika rasmi ndoto za Taifa Stars kushiriki Kombe la Dunia 2026 kwani Taifa Stars haitoweza kumaliza ikiwa miongoni mwa timu nne zitakazomaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi ambazo zinasaka nafasi moja ya kucheza mechi za mchujo za kuwania kufuzu fainali hizo na timu kutoka mabara mengine.

Katika mchezo huo, Taifa Stars itamkosa nahodha Mbwana Samatta ambaye hakuwa miongoni mwa wachezaji waliotajwa kuunda kikosi cha timu hiyo kutokana na majeraha.

Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema kuwa hakuna lengo lingine zaidi ya kupata ushindi.

“Hatuna chochote tunachokihitaji zaidi ya kupata ushindi. Ni mchezo mgumu lakini tutawakabili Morocco bila hofu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Morocco.

                                P             W            D             L              GF          GA          Pts

1.Morocco          4              4              0              0              12           2              12

2.Niger                 4              2              0              2              6              4              6

3.Tanzania           3              2              0              1              2              2              6

4.Zambia              4              1              0              3              6              7              3

5.Congo                               3              0              0              3              2              13           0

6.Eritrea               0              0              0              0              0              0              0

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *