
Baada ya wiki mbili zilizopita kukosa fursa ya kuichezesha mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba kutokana na mchezo huo kuahirishwa, refa Ahmed Arajiga leo atakuwa na kibarua kigumu cha kuamua vita ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kupitia kundi G.
Mchezo huo ambao Arajiga atashika kipyenga leo utafanyika katika Uwanja wa Francistown, Botswana ambao utazikutanisha timu mwenyeji Botswana na Algeria.
Ushindi wa mabao 3-1 ambao Msumbiji iliupata dhidi ya Uganda jana, Machi 20, 2025 huko Misri, umeufanya mchezo huo wa leo ambao utachezeshwa na Arajiga kuwa mgumu na wenye ushindani zaidi.
Matokeo hayo yameifanya Msumbiji kukaa kileleni mwa kundi hilo ikifikisha pointi 12 baada ya mechi tani ikifuatiwa na Algeria yenye pointi tisa huku nafasi ya tatu wakiwepo Botswana wenye pointi sita.
Hii inamaanisha kwamba iwapo Algeria itapata ushindi katika mchezo wa leo, itafikisha pointi 12 ambazo zitaiweka Algeria kileleni mwa msimamo wa kundi hilo kwani itabebwa na kigezo cha kupata matokeo mazuri kwenye mechi yake dhidi ya kinara Msumbiji.
Lakini kama Algeria itapoteza mchezo huo, Botswana itafikisha pointi tisa na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo na hivyo kuweka hai matumaini yake ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
Kupoteza mechi hiyo hapana shaka kutaiweka Algeria katika presha kubwa kwani kitazidi kupunguza uwezekano wake wa kujihakikishia kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tano baada ya kufuzu katika fainali za 1982, 1986, 2010 na 2014.
Katika mechi ya leo, Arajiga atasaidiwa na marefa wawili wasaidizi Kassim Mpanga na Said Hamdani huku refa wa akiba akipangwa kuwa Salum Nasir.