Dakika 810 za maajabu JKT Tanzania

MAAFANDE wa JKT Tanzania ambao waliibania Yanga juzi, Jumatatu wamefikisha dakika 810 katika michezo tisa waliyocheza msimu huu wa 2024/25 huku wakiweka rekodi ya kuwa timu pekee ya Ligi Kuu Bara ambayo haijapoteza katika mashindano yote kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Katika michezo hiyo tisa mmoja ni wa Kombe la FA ambao ni dhidi ya Igunga United (5-1) na mingine ni ya ligi dhidi ya Yanga (0-0), Mashujaa (0-0), Pamba Jiji (0-0), Tanzania Prisons (1-0), Tabora United (4-2), Coastal Union (2-1), KMC (0-0) na Azam FC (0-0).

Matokeo hayo, yameifanya JKT Tanzania kuvuna pointi 14 katika ligi, pia kutinga hatua ya 32 ya kombe la FA ambayo watacheza dhidi ya Biashara ya Mara wakiwa nyumbani hapo hapo kwenye uwanja wao wa Meja Jenerali Isamuhyo ambao umekuwa mgumu kwa wapinzani wao.

Kati ya timu tisa ambazo imecheza nazo kwenye uwanja huo, ni tatu tu ambazo zimepata bao ambazo ni Igunga United, Tabora United na Coastal Union, vigogo wa soka la Tanzania, Yanga na Azam ambao wanaonekana kuwa na safu kali za ushambuliaji, wameambulia patupu.

Akiongelea kiwango chao katika uwanja wa Isamuhyo, kocha wa JKT Tanzania,  Ahmed Ally alisema; “Tumekuwa na wakati mzuri nyumbani na hili ni jambo la kujivunia lakini naamini kuwa bado tunakazi ya kufanya ili kuwa bora zaidi. Tutaendelea kufanya kazi mapungufu yetu.” 

Ally atakuwa na kibarua kingine katika mchezo ujao wa ligi, Februari 13 na wataikaribisha Isamuhyo, Singida Black Stars iliyotoka kutandikwa kwenye uwanja wa Manispaa Mwenge dhidi ya KMC kwa mabao 2-0.

Wakati JKT Tanzania ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza kwenye uwanja wake wa nyumbani, waliotandikwa sana ni Dodoma Jiji, Namungo na Tanzania Prisons kila mmoja amepoteza mara nne. Kwa upande michezo ya ugenini, Simba na Yanga ndio timu pekee ambazo bado hazijapoteza.

Katika michezo tisa ambayo Simba imecheza ikiwa ugenini imeshinda nane na kutoa sare moja hivyo imekusanya pointi 25, Yanga imecheza michezo minane ugenini, imeshinda saba na kutoa sare moja, imekusanya pointi 22.

Kengold ambao wanapambana kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja ndio timu ambayo imechapwa katika michezo mingi ya ugenini (10).

Hawajavuna pointi yoyote wakiwa ugenini, zaidi wameruhusu mabao 24.