
Pamoja na kutanguliwa mabao mawili, Tanzania Prisons imetumia dakika 15 kufanya ‘comeback’ na kuifumua JKT Tanzania mabao 3-2 kuendeleza matumaini ya kubaki salama Ligi Kuu.
Mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kila timu ilihitaji ushindi, huku Prisons wakiwa ndio wenye uchu wa alama tatu zaidi kutokana na nafasi waliyopo.
JKT Tanzania ndio walitangulia kupata mabao mawili dakika ya 11 na 41 kupitia kwa Mohamed Bakari yaliyodumu hadi mapumziko.
Prisons ilionekana kutulia na kufanya mashambulizi zaidi, huku Michael Mhilu aliyeibuka mchezaji bora wa mechi akionyesha uwezo mkubwa kuiamsha timu hiyo na kuweza kusawazisha mabao hayo kisha kupata la ushindi.
Oscar Mwajanga ndiye alianza kuwainua mashabiki wa Prisons dakika ya 77, Jeremia Juma akipachika la pili dakika ya 80 na Mwajanga kurejea tena wavuni dakika ya 89 na kuwahakikishia ‘Wajelajela’ alama tatu.
Huo unakuwa ushindi wa tatu mfululizo kwa maafande baada ya awali kuwanyoa Kagera Sugar bao 1-0, Ken Gold mabao 3-1 na leo tena wanatakata kwa ushindi huo na kuchumpa nafasi ya 14 kwa alama 27.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amesema kujituma kwa wachezaji wake ndio siri ya mafanikio na kuwa kampeni yao ni kuona kila mchezo wanapata alama tatu.
Amesema michezo mitatu iliyobaki dhidi ya Coastal Union, Yanga na Singida Black Stars ni ya kimkakati ili kuhakikisha wanaendelea kushinda na kujinasua nafasi za chini.
“Mechi ilikuwa ngumu, lakini baada ya kuwasoma wapinzani tukaja na mfumo tofauti kuwakimbiza kupeleka eneo lako na tukaweza kusawazisha na hatimaye kupata la ushindi.
“Bado hatuko eneo zuri hivyo tunaenda kusahihisha makosa ili michezo inayofuata mitatu tushinde yote, lengo ni kumaliza nafasi nzuri na kuwa salama,” amesema kocha huyo.