
KATI ya mambo ambayo wachezaji wa Simba na Yanga wanapenda kuyafanya katika maisha yao ya soka ni kucheza mechi za ushindani hasa Kariakoo Dabi.
Mechi hizo zina heshima yake kama ukifanikiwa kufanya vizuri, lakini ikiwa tofauti inaweza kukuharibia.
Kuna mifano ya wachezaji wengi ambao kupitia Kariakoo Dabi maisha yao ya soka yalipaa kwa kasi, huku wengine yakishuka kwa kiwango cha SGR.
Unamkumbuka Shiza Kichuya, kiungo mshambuliaji ambaye kwa sasa anaitumikia JKT Tanzania? Aliimbwa sana kutokana na tukio lake la kufunga bao la kusawazisha kwa kona ya moja kwa moja na kupewa jina la Kichuya Kona.
Hiyo ilikuwa Kariakoo Dabi iliyochezwa Oktoba Mosi, 2016 katika sare ya 1-1, Kichuya akisawazisha dakika ya 87 baada ya Amissi Tambwe kuipa uongozi Yanga dakika ya 26.
Wakati Kichuya kwake ikiwa ni shangwe kupitia Kariakoo Dabi, Hussein Kazi na Kelvin Kijiri ni kama kwao mambo yameharibika kabisa.
Dabi ya mwisho iliyochezwa Oktoba 19, 2024, Kijiri alijifunga katika dakika ya 87 na kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Kabla ya hapo, Hussein Kazi alionekana kuchangia Simba kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Aprili 20, 2024 baada ya kuingia mapema kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Henock Inonga, kisha kumchezea faulo Aziz Ki katika dakika ya 18 na Yanga kupata penalti iliyofungwa na Aziz Ki mwenyewe.
Matukio hayo mawili kwa wachezaji hao wa Simba, yamewafanya kutopata nafasi ya kucheza kwa muda mrefu jambo linalotoa tafsiri ni kama Kariakoo Dabi zimewatibulia.
Sasa weka kando hayo, njoo kwenye Kariakoo Dabi ya Jumamosi hii ambayo Yanga itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa duru la pili la Ligi Kuu Bara.
Katika dabi hiyo, ukiangalia wachezaji waliopo Simba na Yanga, kuna wengine huoni kabisa nafasi ya wao si kucheza tu bali hata kukaa benchini.
Hiyo inatokana na mwenendo wao ulivyo msimu huu baada ya kupoteza namba mbele ya wale wanaofanya vizuri. Kwa maneno mafupi, unaweza kusema dabi hii kwao imewakalia kushoto.
Hussein Abel na Aishi Manula, ni magolikipa ambao dabi hii kucheza kwao labda itokee miujiza, lakini kwa uhalisia hakuna nafasi kwao, huku Ayoub Lakred jina lake likiwa limeondolewa katika usajili licha ya kuendelea kufanya mazoezi na timu hiyo ya Msimbazi.
Hiyo inatokana na kwamba msimu huu katika mechi zote 30 za kimashindano ambazo Simba imecheza, Ligi Kuu (21), FA (1) na Kombe la Shirikisho Afrika (8), makipa hao hawajapata hata dakika moja ya kucheza.
Kocha Fadlu Davids amekuwa akimtumia zaidi Moussa Camara aliyecheza mechi 28, wakati Ally Salim akicheza mbili kati ya 30, moja ya Ligi Kuu na nyingine FA.
Mchezo uliopita wa ligi ambao Simba iliifunga Coastal Union mabao 3-0, Ally Salim alidaka wakati Camara akipumzishwa kutokana na kupata maumivu. Benchini alikuwapo Hussein Abel.
Ishu ya Lakred kutopata nafasi ya kucheza hata mechi moja ya kimashindano msimu huu inatokana na majeraha makubwa aliyoyapata mwanzoni mwa msimu huu na kuondolewa kwenye mfumo huku akibaki kufanya mazoezi pekee, wakati Aishi Manula aliyecheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Al Hilal Agosti 31, 2024 ambayo kipindi cha pili aliingia Hussein Abel, naye hachezi licha ya kwamba awali alikuwa majeruhi na sasa amepona na amewahi kukaa benchini ikiwamo katika mechi za kimataifa.
Ukiachana na eneo la golini, katika ulinzi Hussein Kazi ambaye ni beki wa kati na Kelvin Kijili anayecheza beki wa kulia, wana nafasi ndogo ya hata kukaa benchini kesho kwani nafasi zao kuna watu waliojijengea ngome yao ambao ni Shomari Kapombe na David Kameta upande wa beki wa kulia, wakati Chamou Karabou, Abdulrazack Hamza na Che Fondoh Malone wakicheza pale kati.
Eneo la kiungo lenye wachezaji wengi wanaompa wakati mgumu Fadlu kuwapa nafasi, kuna Mzamiru Yassin na Omary Omary ambao kwao kucheza mechi hii wana nafasi ndogo sana kutokana na rekodi zilivyo.
Omary amecheza mechi mbili tu za ligi kati ya 21 na hakuna aliyofikisha zaidi ya dakika 35, wakati Mzamiru ambaye yupo na kikosi hicho tangu 2016, amecheza mechi saba za ligi msimu huu akipoteza nafasi mbele ya Yusuph Kagoma na Fabrice Ngoma ambao Fadlu anawatumia zaidi kwa sasa.
Augustine Okejepha naye nafasi ya kuanza ni ndogo lakini kuna uwezekano akakaa hata benchini kwani mara kadhaa amekuwa akisaidia akianzia nje.
Edwin Balua na Joshua Mutale wanaocheza eneo la kiungo wakitokea pembeni, kwa pamoja walianza katika Kariakoo Dabi ya Ngao ya Jamii, baada ya hapo, wamekuwa wakikaa benchini kutokana na washindani wao wanafanya vizuri akiwamo Kibu Denis na Elie Mpanzu.
Valentino Mashaka ni mshambuliaji, anapigania nafasi na Leonel Ateba na Steven Mukwala ambao kila mmoja ana mabao manane, hivyo wawili hao mmoja wao anaweza kuanza kutokana na mfumo wa Fadlu kutumia mshambuliaji mmoja, kisha mwingine akitokea benchini kama ilivyokuwa dabi ya mwisho dhidi ya Yanga akianza Ateba, Mukwala akaingia baadaye.
Kati ya wachezaji 30 waliopo Yanga, kuna nyota 12 ambao suala la kuanza kikosi cha kwanza wikiendi hii ni dogo kama sio halipo kabisa ambao ni Khomeiny Aboubakar, Aweso Aweso (kipa wa U-20), Yao Kouassi, Jonas Mkude, Salum Abubakar, Willyson Chigombo, Aziz Andabwile, Farid Mussa, Shekhan Khamis, Denis Nkane, Nickson Kibabage na Kibwana Shomari.
Hiyo inatokana na kocha Miloud Hamdi katika mechi sita alizosimamia ndani ya Yanga, jinsi kikosi chake anachokitumia zaidi.
Langoni Djigui Diarra ndiye anatumika zaidi, akisaidiwa na Aboutwalib Mshery. Aweso amepandishwa kutoka timu ya vijana, mara kadhaa amekuwa akiishia kukaa benchini baadhi ya mechi lakini Khomeiny tangu mara ya mwisho alipocheza dhidi ya Mashujaa na kuruhusu mabao mawili Yanga ikishinda 3-2, Desemba 19, 2024, hajadaka tena. Msimu huu amedaka mechi tatu za ligi.
Yao ni majeruhi wa muda mrefu, Kibabage na Kibwana nafasi zao wanaanza Chadrack Boka na Israel Mwenda wao wakiwa benchini.
Aziz Andabwile, Farid Mussa na Denis Nkane nafasi kwao ni finyu zaidi hata kukaa benchini wakati Mkude na Salum Abubakar wanayo hiyo nafasi ya kukaa benchini kutokana na ukongwe wao na uzoefu wa kuzicheza dabi hata wakianzia nje.