
MAMBO ni moto kwelikweli! Hivyo ndivyo ilivyo katika Ligi Kuu Bara wakati mashabiki wa soka nchini wakijiandaa na kipute cha mchezo wa Dabi ya Kariakoo inayotarajiwa kupigwa Jumamosi, wiki hii, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Unaposoma habari hii elewa kwamba wababe wa soka wa Tanzania, Simba na Yanga, mastaa wao wapo tayari mawindoni baada ya kutoka kucheza mechi mbili mikoani ambako kila moja alishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo.
Hata hivyo, siku nne kabla ya kupigwa kwa pambano la Dabi ya Kariakoo, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Staphane Aziz KI amewashtua mashabiki wa timu hiyo baada ya kuonekana akichechemea mara alipotua kwenye Uwanja wa Ndege Dar es Salaam akitokea jijini Mwanza na kikosi hicho.
Licha ya kwanza hakuna aliyetilia maanani wakati video ikimuonyesha Aziz Ki akitembea akiwa ameshika kiuno kisha kuingia ndani ya gari lake uwanjani hapo kinyume nyume, lakini kilichoshtua ni tukio la jana kunaswa akitoka ndani ya Hospitali ya Saifee, iliyopo maeneo ya Morocco.
Chanzo cha kuaminika cha Mwanaspoti kilimnasa staa huyo mwenye mabao saba na asisti saba katika Ligi Kuu Bara msimu akiwa ameshikiliwa na mkewe, Hamisa Mobeto, hali iliyozua sintofahamu, ingawa daktari wa timu hiyo, Moses Itutu amewatoa hofu wana Yanga.
SINEMA ILIANZIA HAPA
Asubuhi ya Jumamosi iliyopita, msafara wa Yanga ulirejea jijini Dar es Salaam kutoka Mwanza ilipoenda kucheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji na Aziz Ki alifunga mabao mawili kipindi cha pili baada ya awali, beki wa kushoto, Chadrack Boka kutangulia mapema kipindi cha kwanza.
Aziz alinaswa na Mwanaspoti kwenye Uwanja wa Ndege, ambapo alionekana kila mara akijishika mgongo na wakati mwingine kiuno na alipoulizwa na Mwandishi wa gazeti hili, alisema anahisi maumivu makali ya kiuno.
Hata hivyo, Aziz KI hakupenda kufunguka sana alipokuwa anadodoswa, zaidi ya kuingia katika gari lake kinyume nyume na kuondoka kusepa zake, akiacha maswali pengine ni uchovu wa mechi au safari, lakini jana Jumatatu, nyota huyo alionekana akitoka hospitali ya Saifee akiwa anachechemea akishikiliwa na mkewe, Hamisa Mobetto.
Mwanaspoti lilimnasa nyota huyo saa 5:30 asubuhi akiingia na mkewe ambaye ni mwanamitindo akiwa na mwendo wa kusuasua na baada ya robo saa alitoka akiwa ameshikwa mkono na mkewe huyo huku akitembea kama mtu mwenye maumivu flani.
Kwa mwonekano, Aziz Ki alikuwa akichechemea na kutembea taratibu mithili ya mtu anayepata maumivu katika nyonga zake, hivyo mkewe alitumia dakika mbili kutoka naye ndani hadi kuingia katika gari aina ya Range Rover lililokuwa limeegeshwa nje ya hospitali hiyo.
KLINIKI SIKU TATU
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya hospitali hiyo, kinasema kuwa Aziz KI amekuwa akihudhuria hispitalini hapo kwa muda wa siku tatu kila siku asubuhi na jioni kwa ajili ya matibabu.
“Ni kweli amekuwa akija hapa kwa siku ya tatu leo akitibiwa jengo la tibaa ya mazeozi (Physiopherapy
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, Aziz Ki amekuwa akionekana hospitalini hapo siku tatu mfululizo akifika na kuelekea katika eneo la tiba mazoezi (Physiotherapy),” kimesema chanzo hicho.
Mmoja ya watu wa karibu wa nyota huyo raia wa Burkina Faso, aliliambia Mwanaspoti, Aziz KI huwa anaitumia hospitali hiyo, kwa vile ana daktari wake maalum anayemsaidia kwa ishu zake za kitabibu.
“Ni maumivu tu ya mgongo ndio yanayomsumbua ndio maana ameonekana hospitalini kwa siku kadhaa ila hali yake sio mbaya kwa sasa,” kimesema chanzo hicho, bila kufananua zaidi hata kilipobanwa na Mwanaspoti.
MSIKIE DAKTARI
Mwanaspoti lilimsaka Daktari wa Yanga, Dk Moses Itutu na kuulizwa juu ya mchezaji huyo kuonekana hospitali ya Saifee, amesema yatakuwa ni masuala yake binafsi na hana taarifa za kuumia kwake.
Yanga iliwapa mapumziko wachezaji wote na jana ndio walikuwa wakiungana tena kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaopigwa Jumamosi kuanzia saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Huenda ameenda hapo kwa masuala yake binafsi au labda amemsindikiza mtu tu,” amejibu Dk Itutu, lakini alipoelezwa namna alivyokuwa anatembea akiwa ameshikiliwa na mkewe alijibu kwa ufupi; “Mimi kama daktari wa timu sina taarifa ya kuumia kwake na wakati huu tunajiandaa na mechi ya Dabi ya Kariakoo, najua ni Yao Kouassi ndiye mchezaji mwenye tatizo, akiwa chini ya uangalizi kwa sasa.”
ALICHOSEMA AZIZ KI MAPEMA
Kabla ya taarifa hiyo mpya wa Aziz Ki kuonekana kama mgonjwa hospitalini, mapema nyota huyo alizungumza na Mwanaspoti na kuweka bayana anavyouona mchezo huo ukiwa wa presha kubwa kwa watani wao, Siomba kuliko Yanga, japo alisema mechi kubwa kama hizo huwa hazitabiriki.
Aziz ambaye ameitumikia Yanga kwa misimu mitatu kiwa miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuamua mechi kubwa, akikumbukwa kwa bao alililofunga msimu wake wa kwanza katika sare ya 1-1 akiisawazishia bao baada ya Augustine Okrah kuitanguliza Simba bao la mapema.
Rekodi zinaonyesha katika kipindi chote alichoichezea Yanga, Aziz KI amecheza dabi tano za ligi na kuhusika katika mabao manne, akifunga matatu na asisti moja na akiizungumzia dabi hiyo, alisema katika maisha ya soka anafurahia zaidi kucheza mechi kubwa, hivyo hakuna anachokihofia.
Alisema, mwanzoni mwa msimu kikosi chao kilipitia changamoto, ila baada ya kuingia mzunguko wa pili wamerejea kwa kasi ya ajabu,jambo ambalo ni hatari kwa wapinzani wao kwani wamewazidi kwa upande wa rekodi.
“Dabi ni mechi ambazo napenda kuzicheza, hivyo mipango yangu ni kufanya kazi ya kuisadia timu yetu kupata ushindi kama kawaida.
“Yanga haina presha kuelekea mchezo huu, ila wapinzani ndio wanayo, kwani wanakwenda kutafuta ushindi ili wazidi kulifuata taji la ubingwa. Nitaingia katika mchezo huo kwa lengo moja tu la kuzingatia ushindi kwa timu yangu, hasa mashabiki wetu na hilo ni lazima tuupate kwani kikosi chetu kiko vizuri kila eneo.”
Katika mchezo wa 114 wa Ligi ya Bara tangu 1965, Yanga ndio wenyeji na ikitambia rekodi ya kuifunga Simba katika duru la kwanza kwa bao 1-0, lililotokana na beki Kelvin Kijili kujifunga.
Msimu wa Kwanza
Yanga 1-1 Simba 1-1
Alifunga bao dk 45+2
Msimu wa Pili
Simba 1-5 Yanga
Alifunga baoa moja dk 73, asisti dk 63.
Yanga 2-1 Simba
Alifunga bao moja dakika 19