
Dar es Salaam. Imebaki kwa watia nia wa Chadema, kuamua ni jukwaa gani la kisiasa wanaweza kulitumia ili kutimiza malengo yao ya kugombea nafasi za ubunge, baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuungana na vyama vingine kuwakaribisha.
Mbali na watia nia ambao walikuwa wamedhamiria kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia Chadema na kulazimika kuachana na wazo hilo ili kuunga mkono ajenda ya kudai mageuzi ya No reforms, no election. Kundi la G55 ni la wanachama wa Chadema wanaopingana hadharani na ajenda hiyo, ambapo walieleza wanakubali mabadiliko, lakini siyo kuzuia uchaguzi.
Kabla ya wito wa CUF, watia nia hao waliwahi kukaribishwa Chama cha ACT- Wazalendo kwa kile kilichokuwa kinaelezwa na viongozi wake jukwaa hilo ni sehemu mbadala kwa wanasiasa wanaoona mambo hayako sawa kwenye vyama vyao.
Hata hivyo, si watia nia wa Chadema wala kundi hilo walioweka wazi mpango wa kwenda chama chochote.
Viongozi wa ACT- Wazalendo kwa maana ya Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu na Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe wamewaeleza wanachama wa Chadema wakiwamo watia nia kuwa wasivunje madirisha milango ipo wazi kujiunga na chama chao.
Aprili 16, 2025, kupitia akaunti ya mtandao X, Zitto aliandika, “Kwa wale wanasiasa ambao wanataka kufanya siasa, lakini milango imefungwa kwenye vyama vyao, wasivunje madirisha wala nyumba! Karibu@ACTwazalendo tufanye Siasa.
“Tunaweza kuleta mageuzi tukiwa mchezoni. Uchaguzi ni jukwaa la kuelimisha na kuamsha umma (mobilization). Uchaguzi ni jukwaa la kuionyesha dunia tunachopigania (exposing the flaws),” aliandika Zitto.
Leo Jumapili, Aprili 20, 2025, CUF inayoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba imejitosa kwa ‘kutupa ndoano’ ya kuwahitaji ili kujiunga nao.
Taarifa kwa umma ya CUF iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mohamed Ngulangwa imesema milango ya G55 kujiunga na chama hicho kama wanaamini kushiriki uchaguzi ni jambo bora.
“Kwa uzito wa kipekee, tunatoa wito kwa wanachama wa Chadema, hususan wale wa G55 na wengine wanaoamini kwamba kushiriki uchaguzi ni bora kuliko kususia, waje CUF- Chama Cha Wananchi ili tuendeleze mapambano,” amesema Ngulangwa.
“Tunarudia kutoa wito kwa wananchi kuendelea kujiunga na chama chetu ili kuongeza nguvu ya kupambana “jino kwa jino” dhidi ya watumishi watakaojaribu kudhulumu haki ya wapiga kura kwenye uchaguzi huu,”amesema.
Ngulangwa amesema chama hicho kimefanya tafakuri ya kina na kubaini mapambano ambayo CUF na vyama vingine vya upinzani viliyafanya vikiwa ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi yalikuwa na tija kubwa zaidi kwa Taifa, kuliko walipobaki nje.
Amesema msimamo wao mpaka sasa ni wa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025: “Tunaendelea kujiandaa kuukabili uchaguzi kwa mazingira yaliyopo huku tukiendelea kutoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kukaa chini na vyama vya siasa kuangalia namna ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki.”
“Uchaguzi huru na haki ni njia pekee ya uhakika ya kulinusuru Taifa hili kuingia kwenye machafuko likiwa mikononi mwake,” amesema.
Kufungua pazi la wagombea
Kuhusu ratiba ya kuchua fomu ya kuwania nafasi ya urais, ubunge na udiwani ndani ya chama hicho, Ngulangwa amesema kupitia kikao kinachotarajiwa kufanyika hivi karibu wataweka kalenda ya kuchukua na kurejesha.
“Wanachama wetu wamekuwa wakiulizia siku na utaratibu wa kuchukua na kurejesha fomu. CUF ni taasisi inayoongozwa na vyombo vya kikatiba. Baraza kuu la uongozi la taifa kwenye kikao kijacho kinatarajiwa kuweka kalenda na utaratibu mzima wa kuwapata wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano, urais wa Zanzibar; ubunge, uwakilishi na udiwani,” amesema.
Wakati CUF ikitarajia kuweka ratiba yake tayari vyama vingine vinaendelea na michakato na vingine vimekwisha kuwapata wagombea wa nafasi za urais. Miongoni mwa vyama hivyo ni CCM ambayo imewateua Rais Samia kuwania urais. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuteta nafasi hiyo kwa Zanzibar.