CSR yaleta mvutano RC awatoa nje ya kikao watumishi GGML, nao wajibu

Geita. Mvutano  wa fedha za uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) umeibuka katika kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Geita (CSR) hali iliyosababisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella kuwatoa nje watumishi watatu wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita(GGML).

Kiini cha mvutano huo ni Sh9.2 bilioni zilizopaswa kutolewa na Kampuni ya GGML kwa mwaka 2024 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo hadi sasa hazijatolewa.

Awali Meneja mwandamizi wa GGML kitengo cha uendelezaji, Gilbert Moria alikieleza kikao kuwa mwaka 2024 kampuni hiyo iliwasilisha mpango wa Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita Februari 2024 na kupelekwa wizarani na kibali kilitoka mwishoni mwa Novemba 2024.

Amesema kama kampuni  waliona kutekeleza mpango huo kwa mwezi mmoja haikuwa rahisi na tayari Tume ya madini imewaandikia barua  ikitaka mpango wa mwaka  2025 ambapo wao kama kampuni walipanga kutumia mpango wa 2024 uwe wa 2025 kwa manispaa ya Geita na hadi sasa ule wa Wilaya ya Geita bado haujapitishwa.

Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya mwanasheria wa GGML, David Nzaligo kudai mpango huo ulichelewa kupitishwa na halmashauri hivyo fedha za 2024 hazipo,kitendo kilichomkera Mkuu wa Mkoa na kuwaamuru watoke nje .

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akizungumza kwenye Kikao cha Ushauri cha Mkoa ambacho pamoja na mambo mengine kilijadili masuala ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Msilete mchezo hakuna biashara ya ujanjaunja Sh9 bilioni za wananchi mnataka kuzichukua hivihivi yaani kweli manajimenti yote mmekaa mmekubaliana kufanya hivi tokeni muendelee na kazi zenu, siku mkizirudisha ndio mtakuja hapa mnajijengea himaya ya kwenu mnatengeneza utaratibu wenu,”amesema Shigella.

“Hivi tusipowapa ‘sapot’ yetu mtafanya kazi hapa mgodini? Gao wananchi wanaosubiria maendeleo nyie mnakaa kwenye bodi mnasema halmashauri imechelewa kupitisha hiyo hela haipo, sasa tokeni mpaka mtuletee fedha ndio mtakanyaga hii ofisi kama hamleti hela ya wananchi msije ofisini kwangu nendeni Tamisemi na kwingine sio kwangu”amesema

GGML yatoa ufafanuzi

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia masuala ya ubia na

uendelevu kwa nchi za Afrika, Simon Shayo ameeleza kuwa Sheria ya madini ya mwaka 2010 kifungu cha 105 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 na kanuni za mwaka 2023 imeipa kampuni zinazomiliki leseni ya uchimbaji(SML) wajibu wa kuandaa mpango wa wajibu kwa jamii (CSR).

Wajumbe wa kikao cha Ushauri cha Mkoa.

Amesema mpango huo unapaswa kuzingatia mahitaji,kiuchumi,kimazingira na tamaduni za jamii husika, mpango uliandaliwa na kampuni kwa kushirikiana na jamii husika na kuwasilishwa kwa Halmashauri ya mji na  Wilaya ili kuridhiwa na mamlaka kisha kushauriana na Wizara ya Fedha na Tamisemi.

Amesema GGML iliwasilisha mpango wake wa CSR kwa Halmashauri za Wilaya na Mji Februari 2024 haukuridhiwa na halmashauri wala wizara zilizotajwa hadi Novemba 2024.

Amedai hadi sasa GGML haijapokea taarifa yoyote rasmi ya Manispaa ya Geita kuifahamisha ili waandae  mpango wa utekelezaji na kuendelea  kutekeleza miradi itakayokuwa imekubaliwa na pande zote mbili.

Amesema kampuni hiyo iko tayari kutekeleza mpango wake wa CSR kama ilivyopendekezwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika kama ilivyo matakwa ya sheria na kanuni za CSR kwenye sekta ya madini.

Mbunge wa Chato, Merdad kalemani amesema CSR ni takwa la kisheria kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu cha 105 na kwa mujibu wa kanuni ya CSR ya 2023 inapaswa kulipwa kila mwaka.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu  amesema GGML kwa mujibu wa sheria wanapaswa watekeleze CSR ya mwaka husika kabla ya mwaka kuisha na kwamba majibu ya kuidhinisha mpango kazi yalipitishwa mwaka jana na walielezwa walete mpango kazi wa 2025, lakini hadi sasa hawajaipeleka.

Amesema kitendo GGML kudai wamefuta mpango wa 2024 sio sahihi kwani wao huona CSR ni msaada lakini ukweli sio msaada na kuwataka waombe radhi kwa kudharau mamlaka.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema changamoto kubwa iliyopo kwenye utekelezaji wa miradi ya CSR ni kuchukua muda mrefu bila kufanya maamuzi,huku akidai GGML imekuwa na gharama kubwa za utekelezaji wa miradi tofauti na ile inayotekelezwa na Serikali.

“Unaenda kwenye mradi chumba kimoja kimegharimu Sh40 au Sh35 milioni ghama hizi hata wannachi wanahoji wafike mahali kwakuwa dhamira ni njema tutengeneze mfumo tunaposubiria kanuni tuwe na gharama za ujenzi zinazofanana, lakini pia miradi yao haikamiliki kwa wakati hili walitazame muda  wa utekelezaji ni mkubwa mno,”amesema Komba.