CRDB yapeleka wafanyabiashara maonyesho ya biashara China

Yiwu, China. Katika kuendeleza uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Benki ya CRDB imeratibu safari ya wafanyabiashara 36 kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania kwenda kushiriki Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Canton yanayoendelea nchini China.

Maonyesho haya yanawakutanisha wajasiriamali kutoka mataifa mbalimbali duniani, kuwapa fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wakurugenzi wa makampuni ya huduma na bidhaa wanazozihitaji na hivyo kupanua uwezo wao wa kuendesha biashara na miradi ya kiuchumi.

Mkuu wa Kitengo cha Uwakala wa Benki ya CRDB, Catherine Rutenge ambaye ni mkuu wa msafara huo, amesema hii ni sehemu ya juhudi za benki kuongeza uelewa wa wateja wao kupitia mafunzo na ziara za kimataifa.

“Wateja wetu watakaa China kwa wiki mbili, watapata muda wa kutembelea viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazopatikana nchini kwetu. Kupitia ugeni huu, wanapata maarifa kuhusu bei, ubora na muonekano wa bidhaa wanazozihitaji kulingana na mahitaji ya wateja wao,” amesema Catherine.

Ameongeza kuwa CRDB kupitia CRDB Bank Foundation hutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo, ikiwa ni pamoja na elimu inayotolewa masokoni na vituo vya mabasi.

Elimu hiyo hutolewa kupitia semina na kushiriki katika maonyesho makubwa kama haya ya Canton.

“Huku dunia nzima inakutana, ni nafasi ya kipekee kwa mtu kujifunza. Tutatumia njia zote zinazowezekana kuwawezesha wateja wetu kuimarisha juhudi za kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Catherine.

Mmoja wa washiriki, Rose Mongo, mfanyabiashara wa magauni na vifaa vya harusi kutoka Karagwe mkoani Kagera, amesema safari hii imemfungulia macho kwa kiwango kikubwa.

“Kwenye hii safari kuna wafanyabiashara kutoka karibu mikoa yote. Leo tumetembelea soko la bidhaa hapa Yiwu, nako nimeona fursa ambazo nisingezifahamu nikiwa nyumbani. Nawashukuru CRDB kwa fursa hii,” amesema Rose.

Rose ana matumaini ya kuanzisha mawasiliano ya moja kwa moja na viwanda vinavyotengeneza vitambaa bora kwa ajili ya biashara yake.

“Ukinunua kutoka kiwandani ni nafuu ukilinganisha na gharama za kufuata mzigo Kariakoo. Mawasiliano haya mapya yatapunguza gharama na kuwapa wateja wangu bidhaa kwa bei nafuu na bora zaidi,” ameongeza Rose.

Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Canton hufanyika mara mbili kwa mwaka katika jiji la Guangzhou (zamani likijulikana kama Canton) tangu kuanzishwa mwaka 1957. Ni maonyesho yenye hadhi ya kipekee duniani, yakihusisha kampuni maarufu kutoka kila kona ya dunia, yakitoa fursa kwa wajasiriamali kushirikiana kibiashara na kutanua mitandao ya ushirikiano wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *