
Kiongozi wa upinzani Tidjane Thiam ameondolewa kwenye orodha ya mwisho ya uchaguzi. Jina la kiongozi wa chma cha PDCI halionekani katika hifadhidata iliyowekwa mtandaoni usiku wa Jumanne, Juni 3 kuamkia Jumatano, Juni 4 na Tume Huru ya Uchaguzi (CEI). Kwa hiyo Tume imetekeleza uamuzi wa mahakama ulioagiza kuondolewa kwa kiongozi huyu wa upinzani. Wapinzani wengine ambao hawapo kwenye orodha ya wapiga kura ni Laurent Gbagbo, Guillaume Soro, na Charles Blé Goudé.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Abidjan, Benoît Almeras
Ili kuelewa jinsi hali ilivyo kufikia sasa, lazima turudi kwenye Katiba. Inahitaji wagombea urais wawe raia wa Côte d’Ivoire pekee. Tidjane Thiam, kiongozi wa Chama cha Democratic cha Côte d’Ivoire (PDCI), chama kikuu cha upinzani, alikuwa na uraia wa Ufaransa tangu mwaka 1987. Alivuliwa uraia wake wa Ufaransa mnamo Machi 20, 2025, miezi minne baada ya marekebisho ya mwisho ya orodha ya wapiga kura. Wengi wamewasilisha malalamiko yao kupinga usajili wake.
Hakuna kukata rufaa
Mwishoni mwa mwzi Aprili, mahakama iliamua kwamba Tidjane Thiam sio tena raia wa Côte d’Ivoire wakati wa kusajiliwa kwake mwaka wa 2022, uamuzi uliotokana na Kanuni za Uraia. Maandishi yanabainisha kuwa mtu mzima wa Côte d’Ivoire anapoteza uraia wake anapopata uraia wa kigeni kwa hiari. Uamuzi huu hauwezi kukatiwa rufaa. Inalazimika kwa tume ya uchaguzi, ambayo inaona kuwa haiwezekani kurekebisha orodha ya wapiga kura tena kabla ya uchaguzi wa urais mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025.
Kwa hivyo Tidjane Thiam sasa hastahili. Kiongozi huyu wa PDCI, ambaye amekuwa Ulaya kwa miezi miwili, ameshutumu katika taarifa “kuondolewa kwake kwenye orodha ya wapiga kura,” ambayo amesema ni “mfano wa Côte d’Ivoire kuelekea ukosefu kamili wa demokrasia.” Ametangaza kwamba atalipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, ambayo maamuzi yake hayalazimishi. Kwa kiongozi wa upinzani, maamuzi kadhaa ya mahakama ya Côte d’Ivoire “yanakiuka haki zake za kiraia na kisiasa.” “Mashambulizi haya dhidi ya demokrasia lazima yakome; serikali lazima ihakikishe uchaguzi huru, wa haki na jumuishi,” ameongeza.
Kikao cha Baraza la Seneti kimesusiwa
Kufuatia hali hii, wajumbe sita waliochaguliwa kwa tiketi ya PDCI katika Bunge la Seneti wamesusia kikao cha mashauriano kukemea hali ya kisiasa “nzito na isiyo na uhakika”. Chama hiki cha upinzani pia kimetangaza kuandaa “maandamano.” PDCI imesema inaahusisha “viongozi wa RHDP kuwajibika kwa hali hiyo kwa kupuuza wito wa mazungumzo ya kisiasa.”
Kwa upande wake, chama tawala, RHDP, kimefutilia mbali ukosoaji huu. Kulingana na wasemaji wake, “Si rais Alassane Ouattara aliyeomba kuondolewa kwa Thiam na Gbagbo.” Wasemaji hao wameongeza kuwa vyama vya upinzani havijaondolewa kwenye orodha ya wapiga kura. Kwa maneno mengine, ilikuwa juu yao kutafuta njia nyingine kwa uchaguzi wa urais.
Wapinzani wengine ambao hawapo kwenye orodha ya wapiga kura: Rais wa zamani Laurent Gbagbo, Waziri Mkuu wa zamani aliye uhamishoni Guillaume Soro, na Waziri wa zamani wa Vijana Charles Blé Goudé. Wote watatu wameondolewa tangu kuhukumiwa kwao na mahakama za Côte d’Ivoire.