Dar es Salaam. Msanii wa Muziki wa Hip-Hop nchini, Conboi amemtaja Marioo kuwa ni msanii namba moja kwake huku akibainisha sababu zinazomfanya kusema hivyo ni kazi nzuri anazotoa.

Mbali na hilo, Conboi anayetamba na ngoma ya ‘Tilalila’ aliyomshirikisha Marioo, ameelezea sababu ya kuchelewa kutoka kwa wimbo huo licha ya kutangazwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi, Conboi amesema kolabo yake na Marioo Conboi ina maana sana.
“Kwangu ina maana kubwa sana kwa sababu Marioo anafanya kazi nzuri, kwangu ni msanii namba moja. Mashabiki wangu walikuwa wanategemea kumuona Conboi akishirikiana na wasanii tofauti tofauti kwa sababu ukiangalia katika katalogi yangu huwezi kuona nimeshirikiana na wasanii wengi.

“Nimekuwa nikifanya Hip-Hop zaidi, lakini kwa hivi sasa nimeona nianze kuwapa watu kwa ‘angle’ tofauti tofauti katika utumbuizaji, muonekano na hata mimi binafsi,” amesema.
Akielezea sababu za Tilalila kuchelewa, Conboi amesema: “Unajua namna ya kutangaza wimbo inatakiwa iwe wiki mbili na zaidi ili ifike kwenye majukwaa yote kwa wakati na kupitiwa vizuri. Ni mambo ya maandalizi ya wimbo tu, lakini pia ukiangalia tulikuwa kwenye Kwaresma na Ramadhani kwa hiyo watu wakiwa katika mfungo inakuwa ngumu ngoma kufanya vizuri zaidi.”

Licha ya mafanikio katika mapambano yake, Conboi amesema bado hana meneja anayesimamia kazi zake.
“Sina meneja mpaka sasa, mtu yeyote ambaye nafanya naye kazi na kushirikiana sio meneja wangu. Lakini namshukuru Mungu vitu vinanyooka kama hivi,” amesema Conboi.