Colombia: Rais Gustavo Petro ataka mawaziri wake wote wajiuzulu

Rais wa mrengo wa kushoto wa Colombia Gustavo Petro amewataka mawaziri wake na maafisa wengine wakuu kujiuzulu, huku kukiwa na mgawanyiko mkubwa katika serikali yake kufuatia mkutano uliogubikwa na mvutano kati ya mkuu wa nchi na mawaziri wake wiki iliyopita.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Nimeomba kujiuzulu rasmi mawaziri na wakurugenzi wa idara za utawala. “Kutakuwa na mabadiliko katika baraza la mawaziri ili kufikia utiifu mkubwa zaidi wa mpango ulioamriwa na watu,” Petro ameandika siku ya Jumapili, Februari 9, kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Rais wa Colombia, aliyeingia madarakani mwaka 2022 akiwa na ajenda kabambe ya mageuzi ya kijamii, amewasuta takriban mawaziri wake wote kwa kukosa maendeleo katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Waziri wa Mazingira Susana Muhamad, ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano kuhusu tabianchi (COP16) mwaka jana, ametangaza mapema leo kujiuzulu baada ya mkutano usio wa kawaida siku ya Jumanne kati ya rais wa kwanza wa mrengo wa kushoto wa Colombia na serikali yake.

Katika mkutano huo, Petro ambaye aliingia madarakani mwaka 2022 akiwa na ajenda kabambe ya mageuzi ya kijamii, aliwakemea takriban mawaziri wake wote kwa kukosa maendeleo katika utekelezaji wa miradi hiyo. “Nimewasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Gustavo Petro na ni uamuzi mgumu,” Muhamad amesema katika mahojiano yaliyotangazwa na kituo cha kidijitali cha Los Danieles.

Kujiuzulu kwake kunafikisha tatu idadi ya wajumbe wa serikali au maafisa wakuu ambao wamejiuzulu kufuatia mkutano wa baraza la mawaziri wa siku ya Jumanne, ambao ulichukua zaidi ya saa tano na kurushwa moja kwa moja kwenye televisheni. Siku ya Jumatano, Jorge Rojas, mkuu wa Idara ya Utawala ya katika ofisi ya rais wa Jamhuri (DAPRE), na Juan David Correa, Waziri wa Utamaduni, walikuwa tayari wametangaza kujiuzulu.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi akiwemo Makamu wa Rais Francia Marquez walilalamikia kuwepo kwenye kikao cha Armando Benedetti mmoja wa watu wa karibu wa Bwana Petro ambaye anachunguzwa kwa makosa ya ufadhili wa kampeni za urais na malalamiko ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Kama tetezi wa wanamke na kama mwanamke, siwezi kuketi kwenye meza ya baraza la mawaziri la mradi wetu unaoendelea na Armando Benedetti,” Waziri Muhamad alihoji, akitiririkwa na machozi, wakati wa mkutano huo. “Rais Gustavo Petro ameamua kumweka Bw. Armando Benedetti katika ikulu ya rais,” amebainisha siku ya Jumapili. “Hili ndilo nililoshutumu na hili ndilo ninaloshikilia,” ameongeza.