Coastal yaachiwa msala wa Simba

Baada ya Yanga kujifua kwa wiki nzima kujiandaa na mchezo w Ligi Kuu dhidi ya mtani wake Simba kisha mechi hiyo kuahirishwa, shughuli sasa imehamia kwa Coastal Union itakayomenyana na mabingwa hao wa Tanzania Bara kwenye Kombe la Shirikisho kesho Machi 12, uwanjani KMC Complex.

Katika rekodi za Yanga kwenye kombe hilo, inaongoza kwa kutwaa taji hilo ambapo tangu mwaka 2015 iliporejea michuano hiyo imeshinda mara nne huku ikiwa bingwa mtetezi. Pili Yanga imeshinda mechi nyingi dhidi ya Coastal Union katika kukutana kwao tangu mwaka 2011.

Mchezo huo wa leo ambao utabeba hali ya ubabe na rekodi, ni wa hatua ya 32 bora ambao ni wa mwisho baada ya jana kushuhudia mechi tatu huku zingine zikichezwa huko nyuma.

Mshindi wa leo atakamilisha idadi ya timu 32 ambazo zitakwenda kupambana hatua ya 16 bora.

Katika mechi 23 za Yanga na Coastal Union walizokutana tangu mwaka 2011, Wanajangwani wameshinda michezo 15 huku Wagosi wa Kaya wakishinda tatu na sare tano. Mara ya mwisho wamekutana Oktoba 26, 2024 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Yanga ikishinda 1-0.

Pamoja na ubabe wa Yanga mbele ya Coastal, lakini timu hizo zilipokutana katika fainali ya michuano hiyo Julai 2, 2022 iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, moto uliwaka huku Wanajangwani wakilazimika kunyakua taji kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 3-3, mechi ikienda dakika 120 kwani dakika 90 ilikuwa 2-2.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga ndani ya muda wa kawaida yalifungwa na Feisal Salum (dk 57), Heritier Makambo (dk 82) na Denis Nkane (dk 113), kwa upande wa Coastal Union yalifungwa na Abdul Suleiman Sopu aliyepiga hat trick dakika ya 11, 88 na 98.

Kwenye mikwaju ya penalti, Yanga walifunga zote nne walizopiga kupitia Yanick Bangala, Heritier Makambo, Dickson Job na Khalid Aucho. Coastal walipiga tatu, wakafunga moja kupitia  Victor Akpan huku Aman Kyata na Rashid Mohamed Chambo wakikosa.

Mbali na hivyo, hatua ya 64 bora ya michuano hiyo, Coastal Union ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Stand FC huku Yanga ikiichapa Copco 5-0.

VIKOSI VYAO

Ukiangalia kikosi cha Yanga kina wachezaji wengi kutoka mataifa mbalimbali wanaozichezea timu zao za taifa, baadhi ni Stephan Aziz Ki (Burkina Faso), Djigui Diarra (Mali), Khalid Aucho (Uganda), Ibrahim Bacca, Dickson Job na Clement Mzize(Tanzania), Clatous Chama na Kennedy Musonda (Zambia).

Coastal Union ambaye kwa sasa anayeitwa kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania ni Lameck Lawi, jambo ambalo wadau wanaona Yanga itakuwa na nafasi zaidi ya kushinda mchezo huo, kutokana na kikosi chao kuwa na wazoefu wengi.

Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah amesema: “Yanga ina wachezaji wengi wanaocheza timu za mataifa yao, tofauti na Coastal ambako kwa sasa kuna Lawi, zamani walikuwepo Abdul Hamisi Suleiman ‘Sopu’ (Azam) na Bakari Mwamnyeto (Yanga).”

Kauli yake haijatofautiana na ya mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma mwenye rekodi ya kufunga mabao 25 katika msimu mmoja wa Ligi Kuu aliyesema Yanga ina nafasi ya kushinda kutokana na uzoefu wake.

“Yanga ina kikosi bora kuliko Coastal ingawa mpira ni dakika 90, lolote linaweza likatokea, kila mchezaji akijitoa kwa ajili ya timu yake, mechi itakuwa ngumu,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *