Coastal Union na mzimu wa hat trick Bara

MTAMBO wa kuzalisha hat trick. Ndivyo unavyoweza kusema kwa Coastal Union kutokana na kuwa na rekodi ya kupigwa hat trick katika mechi zake kadhaa, ikiwamo ya juzi ilipovaana na Simba katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Katika mchezo huo wa juzi ulimshuhudia, nyota kutoka Uganda, Steven Mukwala akifunga mabao yote na kuwa hat trick ya kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Asante Kotoko ya Ghana, lakini ikiwa ni ya tatu katika Ligi Kuu msimu huu baada ya Prince Dube na Stephane Aziz KI wote wa Yanga.

Dube aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Azam, ndiye aliyefungua akaunti ya ‘hat-trick’ msimu huu, wakati kikosi hicho kilipoizima Mashujaa kwa mabao 3-2, Desemba 19, 2024 kabla ya Aziz KI kufuatia Yanga ilipoizuima KMC kwa mabao 6-1 Februari 14, mwaka huu, ikiwa ni ya pili kwa Yanga.

Lakini sasa usichokijua ni Coastal imekuwa kichaka kwa vigogo wa soka hapa nchini, kwani msimu uliopita aliyekuwa nyota wa Simba, Mkongomani Jean Baleke aliifungia pia Simba hat trick katika ushindi wa 3-0, mechi iliyopigwa Septemba 21, 2023.

Msimu wa 2020-2021, aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco anayekipiga kwa sasa JKT Tanzania, aliifunga Coastal hat trick katika ushindi wa mabao 7-0, mechi iliyopigwa Sheikh Amri Abeid Arusha, Novemba 21, 2020.

Hassan Dilunga alianza kuifungulia akaunti ya mabao Simba baada ya kutupia dakika ya nane tu, kisha Bocco kufunga dakika ya 24, 29 na 38, Clatous Chama aliyepo Yanga kwa sasa akafunga mawili dakika ya 62, 85 na Bernard Morrison dakika ya 45.

Msimu wa 2014-2015, Coastal Union ikakutana na kichapo kingine cha mabao 8-0, dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Mrundi Amissi Tambwe ambaye kwa sasa ni meneja wa Singida Black Stars akitupia manne.

Katika mchezo huo uliopigwa Aprili 8, 2015, Tambwe aliyafunga mabao hayo dakika ya 9, 34, 48 na 90, huku Simon Msuva pia akifunga mawili dakika ya 23 na 87, huku mengine yakifungwa na Kpah Sherman dakika ya 50 na Salum Telela dakika ya 88.

Simba pia iliwahi kupata hat trick mbili mbele ya Wagosi walipoinyoa kwa mabao 8-1 mechi iliyopigwa Mei 8, 2019 na Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kila mmoja aliotoka na mabao matatu, huku mengine mawili yakifungwa na Hassan Dilunga na Clatous Chama na Raizin Hafidh aliifungia Coastal.

Hat trick ya juzi iliyofungwa na Mukwala inakuwa ni 24 katika misimu mitano kuanzia 2020-2025, huku Aziz Ki akiongoza akifunga nne, akifuatiwa na John Bocco mwenye tatu, huku Saido Ntibazonkiza, Jean Baleke na Dube wakifuatia kila mmoja akiwa na mbili. Saido na Baleke kwa sasa hawachezi Bara, huku wachezaji 12 akiwamo Mukwala, Adam Adam, Juma Liuzio, Jeremiah Juma, Shiza Kichuya, Idris Mbombo, Ibrahim Mkoko, Fiston Mayele, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Kipre Jr, Wazir Junior na Ismail Mgunda kila mmoja akiwa amefunga moja.

Msimu uliopita, Ligi Kuu ilishuhudia hat trick saba, huku Yanga na Azam zikiongoza kwa kupata mbili, wakati Simba, KMC FC na Ihefu zikipata moja kila mmoja wao.

Msimu uliopita, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliifungia Azam, hat trick katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 4-0, dhidi ya Tabora United, Agosti 16, 2023, kisha Jean Baleke akaifungia Simba ilipoinyuka Coastal Union 3-0, Septemba 21, 2023.

Aziz KI aliifungia Yanga ilipoifunga Azam mabao 3-2, Oktoba 23, 2023, kisha akafunga pia katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Mei 28, 2024 na Kipre Junior akaifungia Azam ilipoinyuka Mtibwa Sugar 5-0, Novemba 24, 2023.

Waziri Junior anayekipiga Al-Mina’a SC ya Ligi ya Iraq, alifunga kipindi akiichezea KMC iliposhinda 4-2  dhidi ya Tabora United Machi 10, 2024, huku, Ismail Mgunda akaifungia pia Ihefu iliposhinda 5-1 na Mtibwa Sugar Mei 28, 2024.

Kocha wa Coastal, Juma Mwambusi alisema sababu iliyowaangusha ni kutokana na wachezaji wa timu hiyo kufanya makosa binafsi, yaliyowapa faida zaidi wapinzani wao na kuwaadhibu kwa idadi kubwa ya mabao nyumbani.

“Tulikosa nafasi kadhaa za kufunga kutokana na kukosa umakini lakini hilo pia lilitokea katika maeneo yote, kwa kifupi hatukuwa na mchezo mzuri, hivyo tunarudi tena uwanja wa mazoezi kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza,” alisema.