Coastal Union na misimu mitatu chonganishi

KIKOSI cha Coastal Union kinajiandaa na mchezo ujao wa Aprili 3, ugenini dhidi ya Kagera Sugar, huku ikiwa bado haiko salama sana kitakwimu katika janga la kushuka daraja, kutokana na pointi 25 ilizokuwa nazo kwenye mechi zake 23.

Katika michezo hiyo iliyocheza, imeshinda mitano, sare 10 na kupoteza minane ikiwa nafasi ya tisa na pointi 25, ambazo zinaweza kufikiwa na timu zilizokuwa chini yake kwa maana ya Mashujaa FC, KMC FC, Namungo, Pamba Jiji na Kagera Sugar.

Timu hiyo ni kama inaendeleza pale ilipoishia kwa misimu mitatu nyuma kwani msimu wa 2021-2022, ilimaliza nafasi ya saba na pointi 38, baada ya kushinda michezo 10 tu, sare minane na kupoteza 12, ikifunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu 31.

Msimu uliofuatia wa 2022-2023 ikaepuka janga la kushuka daraja baada ya kucheza michezo 30, ikishinda minane, sare tisa na kupoteza 13, ikishika nafasi ya 12 na pointi 33, huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 25 na kuruhusu 35.

Baada ya misukosuko mingi, msimu wa 2023-2024, timu hiyo ikajiuliza vizuri baada ya kumaliza nafasi ya nne na pointi 43, baada ya kushinda michezo 11, sare 10 na kupoteza tisa, huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu 19.

Msimu huo uliiwezesha Coastal kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu mara yake ya mwisho iliposhiriki na kuishia raundi ya kwanza mwaka 1989, ikiwa ni mafanikio makubwa ya kujivunia ndani ya timu hiyo.

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo ila misukosuko ikaendelea baada ya kikosi hicho kuachana na aliyekuwa kocha mkuu David Ouma, kwa kile kilichoelezwa na viongozi kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo. Ouma aliachana na Coastal Union Agosti 24, 2024, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ipoteze mabao 3-0, dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Ouma alijiunga na Coastal Union Novemba 9, 2023 akichukua nafasi ya Mwinyi Zahera aliyejiunga na Namungo huku akizifundisha timu za Sofapaka, Mathare United na Posta Rangers.

Kocha huyo aliyetawala soka la Kenya kwa zaidi ya miaka 21, akiwa na leseni ya UEFA, CAF A na uzoefu kutoka kituo cha michezo cha Ajax Amsterdam cha Uholanzi, amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ chini ya Bobby Williams.

Baada ya hapo timu hiyo ikaongozwa na kocha msaidizi, Joseph Lazaro hadi Oktoba 23, 2024, ilipomtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa Mbeya City, Yanga, Ihefu na Singida United, Juma Mwambusi kuchukua mikoba ya Ouma kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Tangu Mwambusi ajiunge na timu hiyo ameiongoza katika michezo 15 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo ameshinda mitatu tu, sare minane na kuchapwa minne, huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 10 na kuruhusu 14.

Kwa rekodi ya misimu mitatu, ni msimu mmoja tu uliopita ambao kikosi hicho kilifanya vizuri hadi kumaliza nafasi ya nne na kufuzu kimataifa, ingawa mingine yote iliyobakia imekuwa ni timu inayopambania kuepuka kushuka daraja.

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni ambayo Mwambusi alifanya na Mwanaspoti, aliweka wazi changamoto kubwa anayoendelea kupambana nayo katika kipindi hiki cha mapumziko ni maeneo yote ya ulinzi na ya ushambuliaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *