
TAARIFA kutoka ilipo kambi ya Coastal Union, zinasema mchezo wao wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumatatu hii dhidi ya Yanga, kikosi hicho hakitaongozwa na kocha mkuu, Juma Mwambusi.
Habari hiyo imekuja siku moja kabla ya timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Mwanaspoti limetonywa, uongozi wa Coastal Union umemalizana na Mwambusi kutokana na matokeo mabaya iliyonayo timu hiyo tangu akabidhiwe.
Mwambusi alijiunga na Coastal Union Oktoba 23, 2024 akichukua mikoba ya David Ouma raia wa Kenya, hivyo amekaa kwa takribani siku 165 hadi Aprili 6, 2025. Kabla ya Mwambusi, kikosi hiko cha Wagosi wa Kaya kilikuwa chini ya Joseph Lazarao ambaye alikaimu kwa muda.
Chanzo cha kuaminika kutoka Coastal Union kimeliambia Mwanaspoti wamefikia muafaka wa kuachana na kocha huyo kutokana na matokeo Mabaya.
“Ni kweli tumemalizana na kocha Mwambusi kwa makubaliano maalumu na hatakuwa sehemu ya mchezo hapo Jumatatu kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, tunaamini ni uamuzi sahihi tulioufanya,” kilisema chanzo hicho.