Clara Luvanga afunga, Al Nassr ikitwaa ubingwa Saudi Arabia

Dar es Salaam. Ushindi wa mabao 3-1 ambao Al Nassr imeupata jana dhidi ya Al Ahli, umeifanya timu hiyo anayochezea Mtanzania, Clara Luvanga kujihajikikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia.

Katika mchezo huo, Clara Luvanga anayeitumikia timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ alifunga bao moja kati ya hayo matatu.

Clara amefunga bao hilo katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza na akachangia bao la pili la timu yake lililopachikwa na Nesrine Bahlouli katika dakika ya 55 huku lingine likiwekwa kimiani na nyota wa zamani wa Simba Queens, Ruth Kipoyi na kuifanya Al Nassr kufikisha pointi 48 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine katika ligi hiyo.

Bao la kufutia machozi la Al Ahli katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Al Nassr Riyadh lilifungwa na Naomie Kabakaba katika dakika ya 26.

Zimebakia raundi mbili ili ligi hiyo msimu huu imalizike na timu inayoshika nafasi ya pili Al Ahli ina pointi 37 ambazo hazitoshi kuifanya iifikie Al Nassr hata kama itapata ushindi katika mechi zote zilizobakia.

Mchango wa Luvanga kwa timu ya wanawake ya Al Nassr haujaishia katika mabao hayo mawili tu aliyochangia katika mchezo wa juzi kwani pia ndiye kinara wa kuifungia mabao timu hiyo msimu huu ambapo hadi sasa ameshapachika mabao 14 katika ligi hiyo.

Hiyo ni mara ya tatu mfululizo kwa Al Nassr kutwaa taji la Ligi Kuu Saudi Arabia kwa wanawake na ndiyo timu inayoongoza kwa kutwaa mara nyingi taji la ligi hiyo.

Kwingineko, nyota wa Tanzania, Hasnath Ubamba na timu yake ya FC Masar wameibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Al Ahli Bank kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Misri ushindi ambao unawafanya kukaa kileleni kwenye msimamo wakiwa na alama 55.

Mtanzania mwingine, Maimuna Kaimu alifunga bao moja akiisaidia timu yake ya Zed FC kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Maadi & Yacht Club.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *