China yaipa Tanzania msaada wa Sh 185 bilioni

Dar es Salaam. Tanzania imepewa msaada wa Sh185 bilioni kutoka Serikali ya China kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na kusaidia programu ya ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu.

Hayo yameelezwa katika hafla wa kusaini mikataba hiyo miwili kati ya Wizara ya Fedha kupitia Waziri wake, Dk Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Dk Nchemba amesema mkataba wa kwanza utahusisha ushirikiano wa kiuchumi na kitaalam wenye thamani ya Sh74.2 bilioni na wa pili ni kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha matibabu na upasuaji wa moyo Afrika Mashariki na Kati ikigharimu Sh111.2 bilioni.

“Lengo la misaada hii ni kuwezesha utekelezaji wa miradi itakayochaguliwa na kukubalika kwa pamoja na Serikali za Tanzania na China, mkataba wa pili una lengo la kujenga Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Magonjwa ya Moyo ya Watoto kwa ajili ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati,” amesema Dk Nchemba.

Amesema msaada wa ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu ni ahadi aliyoitoa Rais wa China, Xi Jinping wakati wa kikao chake na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tisa la Kilele la Ushirikiano wa China na Afrika la mwaka 2024, uliofanyika jijini Beijing.

Amesema msaada wa ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo kwa watoto Mloganzila – unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kama vile upatikanaji wa huduma bora za afya, kukuza uchumi kupitia kuongeza ajira na kuchochea biashara kwa wananchi ili kuboresha maisha yao, kukuza utafiti katika masuala ya afya na elimu na kuendeleza miundombinu.

Balozi wa China Tanzania, Chen Mingjian amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kutokana na ushirikiano wa kihistoria wa muda mrefu na pia imani ya Tanzania kwa nchi hiyo katika kukuza maendeleo ya wananchi.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi kinara yenye ushirikiano bora wa kiuchumi na kijamii na imeshirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya Tanzania – Zambia (Tazara) mradi ambao umekuwa wa kielelezo cha uhusiano huo.

“Pia msaada wa sekta ya afya kupitia JKCI ambao umelenga kunusuru maisha ya watoto wanaougua maradhi ya moyo, pia utakuza ajira na kuwa sehemu ya utalii wa kimatibabu watakaokuja nchini kutoka mataifa mengine,” amesema Mingjian.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge aliishukuru China kwa ufadhili huo utakao kuwa mkombozi mkubwa wa matibabu ya moyo kwa watoto kupitia ujenzi wa Kituo hicho cha Umahiri kitakachojengwa katika Hospitali ya Mloganzila.

Amesema changamoto ya kiafya kwa watoto inayosababishwa na maradhi ya moyo ni kubwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya Watoto 200 wanaozaliwa, wawili wana matatizo ya moyo.

“Hivyo ujenzi wa Kituo hicho cha umahiri utaondoa changamoto ya matibabu,” amesema Dk Kisenge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *