China na Marekani zatangaza mazungumzo ya kibiashara

China na Marekani zimetangaza kuwa zitakutana mwishoni mwa juma lijalo nchini Uswisi kuweka msingi wa mazungumzo ya kibiashara, ya kwanza tangu Donald Trump atoze ushuru wa juu kwa bidhaa za China na Beijing kujibu.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo kati ya Beijing na Washington yatafanyika Uswisi Mei 10 na 11. Hii ni ahadi ya kwanza rasmi ya umma kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani kutatua vita vyao vya kibiashara.

Beijing, hata hivyo, imefafanua kwamba “haitatoa msimamo wake wa kanuni” na “itatetea haki” wakati wa mkutano huu kati ya Makamu wake Mkuu He Lifeng, Waziri wa fedha wa Marekani Scott Bessent na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer, Wizara ya Biashara ya China imeonya leo Jumatano, Mei 7.

Hii ni mara ya kwanza tangu Donald Trump atoze ushuru mkubwa wa forodha kwa bidhaa za China. China na Marekani zimetangaza usiku wa Jumanne, Mei 6, kuamkia Jumatano, Mei 7, kwamba watakutana mwishoni mwa juma lijalo nchini Uswisi ili kuweka misingi ya mazungumzo ya kibiashara.

“Ikiwa Marekani inataka kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo, lazima ishughulikie athari mbaya ya ushuru wa upande mmoja kwa yenyewe na kwa ulimwengu,” Wizara ya China imeongeza katika taarifa. “Iwapo Marekani itazungumza kwa njia moja na kuchukua hatua nyingine, au (…) ikiwa itajaribu kuendelea kulazimisha na kuichafua China chini ya kivuli cha mazungumzo, China haitakubali kamwe.”

“Ninatazamia mijadala yenye tija inayolenga kuweka upya mfumo wa uchumi wa kimataifa ili kuhudumia vyema maslahi ya Marekani,” Scott Bessent amesema katika taarifa yake.

Pande hizo mbili zitakutana Jumamosi na Jumapili kuweka msingi wa mazungumzo yajayo, alisema katika mahojiano na Fox News siku ya Jumanne. “Natarajia tutakuwa tunazungumza juu ya kupunguza mvutano, sio mpango mkubwa wa biashara,” alisema. “Tunahitaji kupunguzwa kasi kabla ya kusonga mbele.”

“Sawa na vikwazo”

Katika jitihada za kuunga mkono uchumi unaolemewa na matumizi duni na vita vya kibiashara na Marekani, Beijing pia imetangaza Jumatano kupunguza kiwango cha riba muhimu na kiasi cha mahitaji ya akiba ya benki ili kuwezesha mikopo. Matangazo ya kiuchumi yameendelea na viwango vya chini vya kukopa kwa wanunuzi wa mara ya kwanza.

Tangu Donald Trump arudi White House mnamo mwezi Januari, utawala wake umeweka ushuru mpya wa jumla wa 145% kwa bidhaa kutoka China, pamoja na hatua mahususi za sekta. Beijing ililipiza kisasi kwa kuweka ushuru wa asilimia 125 kwa bidhaa za Marekani zinazoingia China, pamoja na hatua zaidi zilizolengwa.

Viwango hivi vinachukuliwa kuwa visivyoendelezwa na wachumi wengi, hadi kuongeza hatari ya mdororo wa kiuchumi dhidi ya Marekani na China, na pengine hata kwenda mbali zaidi, hali ambayo ingeambatana na kupanda kwa bei. “Hii si endelevu, (…) hasa kwa upande wa China,” amesema Waziri wa Fedha wa Marekani. “145% na 125% ni sawa na vikwazo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *