Habari kuhusu M23 zimekuwa zinasikika sana katika kipindi cha zaidi ya mwongo mmoja ulipita.
Lakini nini hasa chimbuko la M23? Lilianzishwa lini na kwanini? Je, ni wapiganaji wa DRC? Ni waasi kutoka Uganda na Rwanda walioko DRC? Kwanini Jeshi la DRC linaishutumu Rwanda na Uganda kuwaunga mkono waasi wa kundi hilo katika mapigano yaliyozuka upya wilayani Rutshuru na kusabisha maelfu ya raia kukimbilia nchi jirani ya Uganda?
Kulingana na vyanzo mbalimbali, kundi la M23 lilianzishwa na wanachama wa zamani wa kundi la wanamgambo wa Kitutsi ambao walikuwa wanaungwa mkono na Rwanda na Uganda. Waasi hao walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la Congo chini ya makubaliano yaliosainiwa Jumatatu ya Machi 23, 2009 kwa makubaliano kuwa waweke silaha chini na washirikishwe kwenye siasa za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Chimbuko la M23 lina kiini chake kilichojijenga ndani ya kile kilichofanyika katika tarehe hiyo, Machi 23, 2009.
Hiyo ndiyo siku ambayo kikundi kilichojiita ‘Chama cha Kitaifa cha Ulinzi wa Watu’ (CNDP) kilitia saini mkataba wa amani na serikali ya DRC, ambapo kilikoma kuwa kikundi cha waasi wanaopingana na serikali ya DRC na kuwa chama cha kisiasa, na wapiganaji wake walijumuishwa katika Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC).
CNDP ambacho ni kifupi cha maneno ya Kifaransa (Congrès National Pour la Défense du Peuple) ni kundi la wanamgambo waliokuwa na silaha lililoanzishwa na Jenerali Laurent Nkunda katika eneo la Kivu katika DRC Desemba 2006.
CNDP ilishiriki katika mzozo wa Kivu, mzozo wa silaha dhidi ya jeshi la DRC.
Mwishoni mwa mwaka 2008 kundi hili liligawanyika na Januari 2009 Nkunda alikamatwa na serikali ya Rwanda.

Jenerali Nkunda na kundi lake la waasi la CNDP walikuwa wanaonekana kuwa wanashirikiana na Rwanda katika mzozo wa eneo la mashariki ya Congo.
Kwa muda wa miezi kadhaa Umoja wa Mataifa ulikuwa ukilishutumu jeshi la Rwanda kwa kumsaidia jenerali huyo, ambaye alikuwa akipigana na majeshi ya serikali ya DRC mjini Goma.
Lakini pamoja na mambo yote Alhamisi ya Januari 22, 2009 jeshi la Rwanda lilimkamata Jenerali Nkunda katika eneo la Bunagana, ambalo ni mpaka kati ya mashariki ya Congo na Rwanda, ikiwa ni kolometa 956 kaskazini mwa mji wa Goma.
Kabla ya kukamatwa kulitokea mapambano katika eneo hilo jioni ya siku hiyo. Siku moja kabla ya hapo jeshi la DRC na lile la Rwanda walipambana vikali na waasi mashariki mwa DRC, wakimtaka Nkunda kujisalimisha.
Jenerali Nkunda alikuwa ofisa mkuu katika kundi la waasi la DRC la Rally for Democracy (kikundi cha Goma) baada ya 1998.
Baada ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Congo mwaka 2003, Nkunda alipewa nafasi katika jeshi la serikali ya mpito lakini alikataa kujiunga akihofia kwamba angekamatwa kutokana na uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) dhidi yake, na ndipo alikwenda kuanzisha kundi la CNDP.
Nkunda ambaye aliongoza uasi wa Watutsi mashariki mwa Congo tangu mwaka 2004 na akawa anasakwa kwa uhalifu wa kivita alikamatwa baada ya kujaribu kupinga operesheni ya pamoja ya Congo na Rwanda iliyoanzishwa wiki hiyo kuwasaka wanamgambo wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR wanaoendesha shughuli zao nchini Congo.

Baada ya kutokea mgawanyiko katika kundi hilo mwishoni mwa mwaka 2008 na Jenerali Nkunda kukamatwa mwanzoni mwa mwaka 2009, kikundi kilichosalia cha CNDP, kikiongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, kilipangwa kuunganishwa katika jeshi la kitaifa.
Walioshiriki kumkamata Jenerali Nkunda ni miongoni mwa wale wale wanachama wake wakiongozwa na Jenerali Ntaganda kwa ahadi kwamba wangepewa vyeo baada ya CNDP kuingia mkataba wa amani na serikali ya DRC. Kama ilivyotarajiwa, CNDP na serikali waliingia mkataba huo wa amani Machi 23, 2009.
Tangu hiyo Machi 23, 2009 baada ya kutia saini mkataba huo, Jenerali Ntaganda alikuwa anakaimu kama jenerali katika jeshi la DRC, licha ya kwamba kutafutwa na ICC, na pia alikuwa akivuka mpaka mara kwa mara kwenda Rwanda.
Kulingana na serikali ya DRC, Jenerali Ntaganda alivuka kutoka Goma hadi mji wa Gisenyi, Rwanda, mara mbili mwaka 2011, Machi na tena Septemba, licha ya marufuku ya kusafiri kwake.
DRC iliripoti kwamba katika matukio yote mawili Jenerali Ntaganda alikuwa amekwenda kuhudhuria maziko huko Rwanda, lakini ilikuwa ni baada ya kuomba idhini rasmi ya kufanya hivyo kutoka kwa viongozi wake wa kijeshi na kutoka kwa mamlaka ya uhamiaji.
Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa liliripoti mwishoni mwa mwaka 2011 kwamba Jenerali Ntaganda alidhibiti migodi ya Mungwe na Fungamwaka, karibu na Numbi, kupitia Kampuni ya Great Lakes Mining, iliyosimamiwa na mwanadamu anayeitwa Edson Musabarura.

Jenerali Ntaganda pia alijipatia faida kutokana na uchimbaji wa madini huko Nyabibwe, kupitia muungano wake na Kanali Saddam Ringo ambaye kwa wakati huo alikuwa mmoja wa maofisa wakuu wa waasi.
Huko Rubaya, Jenerali Ntaganda alipata mapato makubwa kutokana na ushuru uliotozwa na polisi wa mgodi. Jenerali Ntaganda aliamuru wanajeshi wake kuingilia kati kwa niaba ya kampuni ya Krall Metal Congo huko Lueshe.
Wakati wote huu yeye alikuwa afisa wa jeshi la DRC baada ya kundi lake la CNDP kuungana na serikali ya DRC. Lakini baada ya muda fulani kupita, yeye na wenzake waliojiunga na jeshi la serikali waliona kuwa mambo mengi waliyokubaliana kwenye mkataba wa amani wa Jumatatu ya Machi 23, 2009 hayatekelezwi. Kama kulipiza kisasi, hapo ndipo waliamua kuasi jeshi DRC na kujitenga nalo. Likabaki kuwa ni suala la muda tu.
Jumatano ya Aprili 4, 2012, iliripotiwa kwamba Ntaganda na wanajeshi kati ya 300 na 600 waliomtii waliasi na kujitoa kwenye jeshi la serikali ya DRC na wakaanza kupigana na vikosi vya serikali katika eneo la Rutshuru kaskazini mwa Goma. Hata hivyo, baadhi ya taarifa zilisema wanajeshi walioasi ni takribani 600.
Kwa hiyo hawa wanajeshi wa kundi la zamani la waasi la CNDP walilikimbia jeshi la Congo, hali iliyozusha hofu katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.
Wanajeshi hao wa ambao walikuwa wamejumuishwa katika jeshi la DRC (FARDC) tangu Machi 23, 2009, waliasi kutokana na amri ya Jenerali Ntaganda, aliyekuwa anaongoza kikosi cha FARDC Kivu Kaskazini.
Siku chache baadaye, Aprili 11, Rais Joseph Kabila wa DRC alisema Ntaganda aliyekuwa anatafutwa na Mahakama ya Uhalifu ta ICC kwa zaidi ya miaka mitano ni lazima akamatwe.
Huo ukawa mwanzo wa kile kilichokuja kujulikana leo kama M23. Aprili 11, 2012, Rais Joseph Kabila wa DRC alitoa wito wa kukamatwa kwa Ntaganda.
Rais Kabila alifanya mikutano ya dharura na maafisa wa juu wa jeshi mashariki mwa nchi kufuatia mamia ya askari kukimbia jeshi la Congo.
Kwa maana hiyo, M23 ilianzishwa rasmi siku ile ile ambayo Jenerali Ntaganda alijitoa kwenye jeshi la serikali ya DRC akiwa na wafuasi wake kati ya 300 na 600, Jumapili ya Aprili 4, 2012, kwa madai kwamba ahadi walizopewa wakati wakitia saini makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009 hazikutimizwa na serikali ya Joseph Kabila.
Hata hivyo, pamoja na kundi hilo la waasi kuanzishwa tarehe hiyo, makeke yalianza kuonekana zaidi miezi miwili baadaye, Juni 6, 2012.
Mambo mengi yalitendeka, yakiwamo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, yalitendeka kuanzia hapo na kuendelea hadi sasa. Je, nini ilikuwa hatima ya Jenerali Ntaganda?
Itaendelea kesho.