Chiesa ageuka mzigo Liverpool

Liverpool, England. Maisha ndani ya Liverpool yanaelekea kuwa mafupi kwa Federico Chiesa kufuatia ripoti kuwa timu hiyo itamtoa kwa mkopo katika kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo kwa vile haijaridhishwa na kiwango chake.

Chiesa aliyejiunga na Liverpool, Agosti 29 mwaka huu, ameonekana kushindwa kumshawishi kocha Arne Slot kumpa nafasi ya kutosha ya kucheza jambo ambalo linaonekana kuwafanya mabosi wa timu hiyo kuanza kufikiria upya juu ya hatima yake klabuni hapo.

Mchezaji huyo amecheza mechi tatu tu kati ya 15 ambazo Liverpool imeshacheza hadi sasa kwnye mashindano tofauti tena kwa dakika 78 sawa na wastani wa dakika 26 tu kwa mchezo jambo linaloashiria kwamba bado hajamshawishi kocha Slot.

Kipaumbele cha Slot kinaonekana kipo kwa  Mohamed Salah, Luis Diaz, Darwin Nunez, Diogo Jota na Cody Gakpo

Na inaripotiwa kuwa Liverpool itakuwa tayari kupokea ofa zinazomuhusu mchezaji huyo ambaye alitamba akiwa na Juventus lakini haitomuuza moja kwa moja bali kumtoa kwa mkopo.

Fursa hiyo ya kumnasa Chiesa kwa mkopo inatajwa kuziweka mkao wa kula timu mbalimbali ambazo zinaripotiwa kwamba zitaichangamkia kwa haraka na kupeleka ofa mezani ili zimpate  winga huyo kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.

Miongoni mwa timu ambazo zinatajwa kutamani kumnasa Chiesa ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Italia, Inter Milan ambayo yenyewe inapanga kupeleka ofa ya kumsajili kwa mkopo wa muda wa miezi sita.

Mwezi uliopita, Slot alisema kuwa sababu inayomfanya asimtumie Chiesa kwenye mechi za timu hiyo ni winga huyo kutokuwa na timu wakati inafanya maandalizi ya msimu ingawa alisema kuwa anaendelea kufanya kazi ya ziada kuhakikisha anaenda sawa na kasi ya wenzake kikosini.

“Kuwa na Fedrico ni rahisi sana lakini ni ngumu mno lakini ni rahisi sana kufafanua.

“Alikosa maandalizi yote ya msimu mpya. nimekuwa nikilisema hili mara kwa mata na kwenda kwenye ligi ambayo kasi yake iko juu kuliko Ligi Kuu ya Italia ina weka ugumu kwake (Chiesa) kuingia katika kasi ambayo timu nzima inayo kwa sasa,” alinukuliwa Slot.

Chiesa alijiunga na Liverpool akitokea Juventus kwa ada ya Pauni 10 milioni ambayo itaongezeka hadi kufikia Pauni 12.5 milioni ikiwa mchezaji huyo ataonyesha kiwango bora.