Chaumma kuwapokea waliohama Chadema

Dar/mikoani. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kitafanya mikutano yake ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kuanzia kesho Jumatatu Mei 19, 2025 jijini Dar es Salaam.

Vikao hivyo vinafanyika baada ya kuahirishwa. Awali, vilikuwa vifanyike Mei 10 na 11, 2025 lakini viliahirishwa. Macho na masikio katika vikao hivyo ni mapokezi ya waliokuwa viongozi na wanachama wa Chadema waliojiuzulu nafasi zao.

Tangu Mei 7, 2025 kumekuwa na wimbi la viongozi na wanachama wa Chadema kutoka maeneo mbalimbali nchini kutangaza kukihama chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kwa madai ya kimepoteza mwelekeo yakiwamo malengo ya kuanzishwa kwake ya kushika dola.

Miongoni mwa waliohama ni viongozi wa kada, mikoa, wilaya, majimbo, kata, waliokuwa wajumbe wa sekretarieti katika utawala wa mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe. Pia, Devotha Minja, aliyekuwa mwenyekiti kanda ya kati naye amekihama.

Waliokuwa wajumbe wa sekretarieti naibu katibu wakuu, Benson Kigaila (Bara), Salumu Mwalimu (Zanzibar), Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema na katibu wa sekretarieti, Julius Mwita.

Aidha, kuna waliowahi kuwa wajumbe wa kamati kuu, wabunge na wanasiasa maarufu ndani ya chama hicho.

Upande wa Zanzibar, wajumbe sita wa sekretarieti nao wameondoka ambao ni Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni Mafunzo, Sera na Uchaguzi, Haji Abeid Haji, Ofisa Utawala na Fedha, Rahima Said Abdallah na Ofisa Utawala, Kassim Abdallah.

Wengine ni Katibu wa Chadema Kanda ya Unguja, Yunus Makame, Katibu wa Chadema Kanda ya Pemba, Habib Ali Khamis na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Asiata Said Abubakar.

Wote ambao wametangaza kuondoka Chadema wamekuwa wakieleza watatangaza wapi wanakwenda kuendeleza harakati zao za kisiasa na Mwananchi limekuwa likiripoti kwamba watakwenda Chaumma.

Chaumma kinachoongozwa na mwenyekiti wake, Hashima Rungwe kinatarajia kujadili masuala mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na kubwa likielezwa ni kuwapokea kundi la wanachama na viongozi waliokuwa Chadema.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka ndani ya Chaumma zinasema: “Kesho tunafanya vikao viwili kwa mpigo cha kamati kuu na mchana halmashauri kuu. Katika Kikao cha mchana ndio tutawapokea hawa jamaa zetu, labda wabadili gia angani lakini kila kitu kipo sawa.”

Chanzo hicho ambacho kimeomba hifadhi ya jina lake kimesema: “Wajumbe wa Halmashauri Kuu tayari wameanza kuwasilia Dar es Salaam, lakini hatujajua ukumbi utakuwa wapi, kwani waandaaji wanafanya siri…bwana aise sisi wenyewe hatujui tunasubiri tu tuambiwe na ndio maana wajumbe wameambiwa waende ofisini kesho asubuhi.”

Alipoulizwa masharti wanayokwenda nayo amesema: “Hawa jamaa wana masharti mbalimbali, wanataka nafasi za juu za uongozi lakini si ya mwenyekiti, kuna wale viongozi ngazi ya kanda, mikoa hadi wilaya waendelee na nafasi zilezile, sasa hili bado tunajadili.”

Mei 11, 2025, Mwita akizungumza katika shughuli ya kujivua kwa wanachama na viongozi wa Mkoa wa kichama wa Temeke jijini Dar es Salaam, alisema Mei 18, 2025 ni siku ambayo watakutana na kuamua rasmi wanajiunga na jukwaa lipi.

“Tujiandae kikamilifu kwa sasa viongozi wenu tunaandaa ukumbi wa kukutana hiyo Mei 18, 2025 tukipata tutawaambia siku hiyo tutavaa na fulana za rangi ya chama tutakachoelekea, tunataka kuwaonyesha kwamba hatujaondoka kwa sababu ya kusaka vyeo,” amesema Mwita.

Leo Jumapili, Mei 18, 2025, Katibu Mkuu wa Chaumma, Mohammed Masoud alipotafutwa na Mwananchi juu ya vikao hivyo amesema maandalizi ya mikutano ya halmashauri kuu na kamati kuu inaendelea vizuri na kesho Jumatatu inafanyika.

“Ni kweli mikutano inaanza kesho lakini bado hatujapata ukumbi kuna watu tumewatuma wanaendelea na mchakato wa kutafuta ‘location’ baadaye tunajua ni wapi tutafanya mikutano yetu,” amesema.

Alipoulizwa inakuaje mikutano inafanyika kesho lakini sehemu ya kufanyika haijulikani amesema: “Kulikuwa na mambo mengi yaliingiliana sasa kama nilivyokueleza kuna watu tumewatuma hadi kufikia muda huo tutakuwa tunajua na tutakuambia.”         

Pia alipoulizwa katika mikutano hiyo wanatarajia kuwapokea makada waliokihama Chadema amesema, “amekueleza nani,” akakata simu.

Akizungumza kuhusu kupokea wanachama wapya waliokihama Chadema, Rungwe amesema, “bado sijajua kama kweli watatokea na tutawapokea katika mikutano hiyo lakini hiyo kesho nitakuambia usiwe na wasiwasi.

Alipoulizwa John Mrema miongoni mwa makada waliokihama Chadema kama kesho wanapokelewa kwanza alianza kujibu kwa kushangaa.

“Wewe umemsikia nani jambo hilo, kama ingekuwa kweli tunapokelewa si taarifa zingeshatangazwa ….Kusema kweli mimi sijui muulize huyohuyo aliyekueleza,” amesema na kukata simu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *