Chaumma kutumia chopa kunadi operesheni yake mpya mikoa 16

Chaumma kutumia chopa kunadi operesheni yake mpya mikoa 16

Dar es Salaam. Chaumma baada ya kuwapokea wanachama wapya, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ametangaza mikakati mipya ikiwemo mwishoni mwa mwezi huu wanatarajia kuzindua operesheni ya C4C Tusonge mbele itakayozunguka mikoa yote.

Operesheni hiyo inayotafsiri ‘Chaumma for Change’, itazinduliwa mkoani Mwanza Mei 30, 2025 kabla ya kuendelea katika mikoa yote nchini kwa siku 16 mfululizo huku kikitumia usafiri wa chopa itakayotumiwa na viongozi waandamizi wa chama hicho.

Mkakati huo umetangazwa leo Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano maalumu wa kuwapokea wanachama wapya kutoka mikoa mbalimbali uliofanyika Ukumbi wa Ubungo Plaza, huku mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe.

“Leo tumelimaliza hili, lakini kuna lingine linakuja ngoma haichezwi mitandaoni, tutaicheza mikoani, naomba niwatangazie rasmi kuanzia Jumamosi ya Mei 30, 2025 ndani ya Jiji la Mwanza tutatangaza operesheni mpya inayoitwa C4C Tusonge mbele,”amesema Mwalimu.

Amesema kwa kuwa watakuwa wanatumia chopa, operesheni hiyo itakuwa inafanyika usiku na mchana kwa ajili ya kupeleka neno la matumaini kwa Watanzania wasihofu, bado Chaumma ina uwezo wa kuwakomboa.

“Nawaomba mjiandae mashine ipo tayari, maana mipango yote iko tayari mnampotoka hapa mkajiandae, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila atawatangazia ratiba baada ya kumaliza tukio hili kikubwa mkaanze kufanya maandalizi,” amesema na kuongeza;

“Hakuna kulala, tuna mashine za kazi, tutawatangazia ratiba ndani ya saa 24, tunaendeleza pale tulipoishia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwalimu amewataka wanachama hao kuungana pamoja katika kukijenga chama hicho kwa wivu mkubwa.

“Tumetoka kwenye kata, turudi kujenga safu za uongozi na taarifa sahihi za wanachama wetu, tumetoka katika majimbo turudi tukayajenge, tumetoka kwenye wilaya na mikoa na Kanda na wengine ngazi ya Taifa na jukumu letu sasa ni kwenda kusuka oganaizesheni za chama chetu kipya,” amesema mtendaji huyo.

Amesema kitu kinachowapa matumaini makubwa, wanachama wote wanayajua mazingira magumu ya kisiasa katika kutafuta haki zao, hivyo wanakoenda wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kukijenga chama na kuwasikiliza wanachama wapya.

“Kuanzia leo hakuna Chaumma mpya wala kongwe, tunatambua tuna kazi kubwa ya kwenda kukijenga chama hiki, lakini binafsi sina hofu wala chembe ya mashaka na kipimo ni hiki kama tumeweza kuelezana na tumefika hivi katika mazingira magumu, ni mtihani tosha,” amesema Mwalimu.

Amesema anatamani kuona ndani ya mwezi mmoja Chaumma inaimbwa kila kata, jimbo, wilaya, mkoa na kanda kwa kuwa wana kila sababu baada ya kujawa na ari na shauku waliyokuwa nayo miaka 20 iliyopita.

Mwalimu amesema kwa kuwa wanashiriki uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu kwa kishindo huku akiwataka wanaohitaji kutangaza nia wafanye hivyo na siku chache zijazo, Kamati Kuu itakutana na kutoa utaratibu.

“Mchakato huu unawahusu na wale wa viti maalumu na niwaambie hakutakuwa na mchakato wa viti maalumu wa kubebana bebana, twende tukafanye kazi na kila mmoja akapimwe kwa kazi yake, hiyo ni njia ya kukifanya chama hiki kubaki na sifa zake baada ya uchaguzi wa Oktoba,” amesema.  

Kwa upande wake Kigaila alipoulizwa kuhusu operesheni hiyo, amesema ratiba itaanza Juni Mosi kwa kuzunguka mikoa yote ndani ya siku 16 kama alivyosema Katibu Mkuu, Mwalimu.

“Katibu mkuu ameshamaliza kila kitu, ziara itaanza Juni Mosi, tunakwenda kwa siku 16 mfululizo bila kupumzika,” amesema Kigaila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *