Chaumma kuhama ofisi, kuteua wakurugenzi wa idara

Chaumma kuhama ofisi, kuteua wakurugenzi wa idara

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeendelea kufanya kufulu kila uchwao, sasa kipo kwenye mchakato wa kutafuta jengo la kisasa litakalosheheni ofisi za watendaji wote wa sekretarieti ya chama hicho ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mbali na hilo, chama hicho ambacho kwa siku za karibuni kimekuwa sehemu ya mijadala maeneo mbalimbali kimesema kuna kundi kubwa la watu wanaotaa kujiunga nacho ili kuwawezesha kuwania udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Chaumma ambacho tangu kuanzishwa kwake miaka 13, makao makuu yake yapo maeneo ya Makumbusho jijini Dar es Salaam ambayo inamilikiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe na haina nafasi ya kutosheleza ofisi za watendaji wote.

Hatua hiyo inatokana na kundi kubwa la viongozi na wanachama waliokuwa Chadema kujiunga na kuteuliwa na Halmashauri Kuu kwenye nafasi za juu ambao ni Salum Mwalimu kuwa Katibu Mkuu, Devotha Minja kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti-Bara na Benson Kigaila kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka ndani ya chama hicho zimeeleza mpango wa chama hicho kutaka kuhama zinatokana na ugeni mkubwa walioupokea kutoka Chadema na kikao cha kamati kuu kinachotarajiwa kufanyika Jumamosi hii.

“Kwa sasa hatuwezi kuendelea kubaki hapa, uwezekano mkubwa wa kuhama upo kwani hawa jamaa wanataka kukijenga chama kuanzia chini hadi juu na huku juu ofisi hii haitoshi ina ofisi chache za watendaji,” amesema mmoja wa viongozi wa zamani wa Chaumma.

Mwananchi imeelezwa kuwa chama kinahitaji jengo angalau litakaloweza kuwa na ofisi saba ikiwemo ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti Bara na Zanzibar, katibu mkuu, naibu katibu mkuu Bara na Zanzibar.

Pia, ofisi za wakurugenzi wa idara zote, ofisa habari na taarifa kwa umma taifa, wajumbe wanane wataalamu walioteuliwa na mwenyekiti kwa kushauriana na ofisi ya katibu mkuu pia makatibu watatu wa mabaraza ya chama (wanawake, vijana na wazee).

Mpango wao unakwenda sambamba na kupata anuani mpya kulingana na mahali walipo lengo kukifanya chama hicho kiwe na ofisi mpya zitakazokuwa na ukumbi wa kukutana na wageni wanaokuja kuwatembelea katika kudumisha mahusiano ya kidemokrasia ya ndani na nje.

Leo, Alhamisi Mei 22, 2025, Mwananchi limemtafuta Kigaila ambaye amesema chama hicho kimeshakuwa kikubwa wanahitaji kupata ofisi mpya ili kuendana na hadhi na haiba ya kimuonekano na yenye kutosheleza watendaji wote.

“Chaumma inaofisi Makumbusho lakini zimeshapitwa na wakati na tumekubalina hilo na tupo kwenye mchakato na jitihada za haraka kupata jengo linaloweza kutosheleza watendaji wote wa kila siku wa shughuli za kichama,” amesema Kigaila.

Kulingana na Kigaila amesema ingawa kipaumbele chao cha kwanza ni kuhakikisha chama hicho kwenye kila kitongoji, kina kuwa na wagombea kuanzia kata na jimbo, lakini kwa kuwa wameshafungua mioyo ya watu ni lazima wawe na ofisi.

“Kuhakikisha sekretarieti inatekeleza majukumu yake ya kila siku, kwa ajili ya mahusiano, kutembelewa na watu lazima tuwe na anuani kwa hiyo tunafanya jitihada ya kupata ofisi inayofanana na Chaumma ya sasa,” amesema Kigaila.

Kigaila aliyekuwa anashilikia wadhifa kama huo kwa kipindi cha miaka mitano Chadema amesema wanahitaji kupata ofisi zaidi ya saba ya katibu mkuu na manaibu wake wawili, wakurugenzi mbalimbali, makatibu wa ngome vijana na wanake wote hao wanahitaji mazingira rafiki kufanya majukumu yao.

“Tunachofanya tunatafuta jengo kubwa litakalowafanya wote hawa wafanye kazi ndani ya hilo jengo, tunapoanza tutapata sehemu ya watu kufanyia kazi,” amesema Kigaila.

Katika hatua nyingine Kigaila amedai baada ya kufanya mkutano maalumu wa kuwapokea wanachama wapya 3,000 waliokihama Chadema amesema baada ya tukio hilo wameanza kupokea maombi mengi ya wanachama wengine kutoka vyama mbalimbali wakitaja kujiunga nao ili wakagombee kwenye uchaguzi mkuu.

“Chaumma ni jukwaa nzuri la kufanyia siasa na kupigania haki za Watanzania na kuna watu makini ambao lengo letu ni kutwaa dola ili tukashawishe maisha ya Watanzania, nikuambie baada ya kishindo cha jana walioleta maombi yakutaka kuja kujiunga nasi ni wengi,” amesema Kigaila.

Amesema milango ya wao kujiunga na chama hicho iko wazi ni wakati wao kwenda kujiunga nao ili wakatimize lengo la kutekeleza ukombozi wa umma wa Watanzania.

Nafasi za wakurugenzi

Chama hicho baada ya kupata uongozi wa juu uliokamilika Mei 19, 2025 katika mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Golden Tulip Masaki, kwa sasa kinajipanga kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa upande wa sekretarieti.

Kamati kuu ya Chaumma inayotarajia kukutana Jumamosi ya Mei 24, 2025 jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengi inaielezwa kutakuwa na uwezekano wa kujazwa na au kuzipanga upya kurugenzi.

“Unajua tuna kurugenzi kama nane hivi na ni chache wenye watendaji, sasa hii kamati kuu ambayo Mwalimu alisema itakutana hivi karibuni inakutana Jumamosi hii na nafikiri sasa inakwenda kuteua wengine,” amesema mmoja wa wajumbe wa kamati kuu.

Mjumbe aliyeomba jina lake lisitajwe, amesema katiba ya Chaumma ya mwaka 2012 toleo la pili mwaka 2024 inabainisha idara mbalimbali kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa na majukumu yake.

Idara hizo ni Uchumi, Fedha na Mipango; Habari na Taarifa kwa Umma; Uchaguzi, Kampeni na Oganaizesheni; Ulinzi na Usalama; Mahusiano na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma.

Zingine ni Idara ya viongozi wa wakilishi wa wananchi kupitia chama; Sheria, Katiba, Haki za Binadamu na Maendeleo ya Jamii.

Kamati kuu hiyo inatarajia kujadili uzinduzi wa operesheni ya C4C tusonge mbele itakayozunguka mikoa yote.  Operesheni hiyo ilitangazwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu.

Operesheni hiyo yenye maana ya ‘Chaumma for Change’ itazinduliwa mkoa wa Mwanza Mei, 30, 2025 na itazunguka mikoa yote ndani ya siku 16 kwa kutumia usafiri wa chopa itakayojumuisha viongozi waandamizi wa chama hicho.

Kinachofanywa na Chaumma kwake haimshangazi kwani ilishatokea hali kama hiyo wakati Augustion Mrema anakihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi amesema Mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza.

“Mrema wakati anahamia NCCR-Mageuzi alikikuta chama kichanga alikuja na wafuasi wake na walitafuta ofisi sehemu zingine, suala la wanachama kuhama ni jambo la kawaida hasa ukiangalia mbeleni kuna tukio la uchaguzi,” amesema Kaiza

Kulingana na Kaiza amesema wengi wao wanatoka Chadema wanaohitaji kugombea kwenye uchaguzi ujao na bila shaka nyuma yao kuna msukumo na ni matarajio yake wataendelea kujiunga wengi na chama hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *