Dar es Salaam. Siku moja baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kupata wanachama na uongozi mpya unaojumuisha waliokuwa makada wa Chadema na wanamuungano wa G55, wadau wa siasa wamesema hatua hiyo itaongeza ushindani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu na kuchochea maendeleo ya demokrasia.
Jana Jumatatu, Mei 19, 2025, kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, kulishuhudiwa wanasiasa Salum Mwalimu, Benson Kigaila na Devotha Minja wakijiunga na chama hicho, wakikabidhiwa vyeo muda mfupi baada ya kukabidhiwa kadi za uanachama.
Hatua ya wanasiasa hao kujiunga na chama hicho ilitarajiwa na wengi, pindi walipotangaza kujivua uanachama wa Chadema kwa nyakati tofauti, kwa kile walichosema hawaridhishwi na mwenendo wa chama hicho.
Katika uteuzi huo uliofanywa na Halmashauri Kuu, Mwalimu aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akirithi nafasi ya Mohammed Masoud Rashid aliyejiuzulu muda mfupi kabla ya kutangazwa mrithi wake.

Mwalimu alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar kabla ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa Januari 21, 2025, uliohitimisha wadhifa wake huo, na baadaye akatangaza kujiondoa katika chama hicho.
Sambamba na Mwalimu, Kigaila aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, akimrithi Kayungo Mohammed aliyejiuzulu sambamba na Masoud.
Kigaila naye aliyekuwa sehemu ya Sekretarieti ya Chadema, akihudumu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu -Bara hadi uchaguzi wa ndani wa chama hicho ulipofanyika, baadaye alitangaza kujiondoa ndani ya chama hicho.
Devotha Minja naye amekaimishwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti-Bara, akirithi mikoba kutoka kwa Rahman Rungwe.
Devotha alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati baada ya uchaguzi wa kanda hiyo.
Viongozi hao wanaunda safu mpya ya Chaumma, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe, aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 18 tangu kuanzishwa kwake.
Hata hivyo, chama hicho kesho kinatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam ambao pamoja na mambo mengine utahusisha kuwapokea wanachama wapya.
Kuongeza ushindani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Jumanne, Machi 20, 2025, wanazuoni wa siasa licha ya kusema kitaongeza ushindani, walionyesha wasiwasi iwapo sera zake mama za miaka yote zitakuwa na uhai kutokana na ingizo jipya la vion
Akizungumzia hilo, mwanazuoni wa historia katika siasa, Philemon Mtoi amesema kwa sababu demokrasia inahitaji vyama vingi, kuamka kwa Chaumma ni sehemu ya kuitikia takwa la demokrasia.
“Ujio wa chama hiki kutokana na kundi la wanachama wa Chadema kuondoka ni muitikio wa takwa la kidemokrasia,” amesema.

Katibu wa Chauma, Mohammed Masoud akitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Kuamka kwa chama hicho, amesema, kutaongeza ushindani wa vyama vingi na kuchagiza maendeleo chanya ya demokrasia.
Hata hivyo, hatua iliyofikiwa amesema inatoa nafasi ya kujua aina ya wanasiasa waliopo nchini, akidokeza,”Hapa tunaangalia political commitment ya wanasiasa. Wapo wale wanaotumia vyama kama vyanzo vikuu vya mapato,” amesema.
Kijamii, amesema Chaumma kitakuwa na wakati mgumu wa kusambaa, kwani msingi wake utajengwa na wanachama ambao taswira zao zinafahamika.
“Kitakosa msingi wa kijamii ambako wanachama ndio walipo, kwani waliohamia na kupata uongozi dhamira yao si ya kuleta mabadiliko katika jamii, bali mabadiliko katika mifuko yao, kwa mtazamo wangu,” amesema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kujiunga na Chaumma kwa viongozi waliokuwa Chadema kuna vitu viwili vinaweza kujitokeza; kwanza, huenda chama hicho kikabadilika hata kama kuna nguvu nyingine ambayo haionekani.
“Tutasubiri tuone, huenda Chaumma kinaweza kuanza kufanya vizuri katika uchaguzi unaokuja. Mbali na hivyo, kama hakuna nguvu nyuma ya msukumo huu, Chaumma tutashuhudia kitakuwa chama kilekile na hata viongozi waliojiunga hawana nguvu ya ushawishi wa umma kivile,” amesema Dk Mbunda.

Amesema wanaodai viongozi waliojiunga na chama hicho hawana ushawishi wana hoja, kwa kuwa hata wakiingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge, hawawezi kufanya jambo kubwa la kuifanya Chaumma ishinde viti vingi.
“Ingawa ni mapema kuanza kuzungumzia hatima ya Chaumma itakuwaje, lakini inaonekana imebadilika kwa sababu imepokea wanachama wapya na kitaanza kuonekana sasa kama chama tofauti na kilivyokuwa,” amesema.
Amesema iwapo Chadema hawatashiriki uchaguzi wa baadaye mwaka huu, huenda Chaumma na ACT-Wazalendo vinaweza kuwa vyama vitakavyotikisa katika uchaguzi mkuu.
Alipoulizwa kama Rungwe anafaa kuongoza jahazi hilo kwa sasa, Dk Mbunda amesema,”Kwa namna yoyote hawawezi kufanya mapinduzi ya haraka hivyo kumtoa Rungwe kama walivyojiuzulu wale viongozi wengine.
“Naamini kuwa makubaliano ni ya ku-accommodate interests za pande zote. Labda swali muhimu kuuliza ni je, Chaumma kitabaki na itikadi ile ile au kitamezwa na itikadi na sera za Chadema kama hao akina Mrema walivyojinadi kufanya?” amehoji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Dk Kanael Kaale ametafsiri hatua hiyo kama ishara ya kuwepo kwa uhuru wa kidemokrasia.

Uhuru huo unatokana na kile alichoeleza kuwa wanasiasa wana fursa ya kuchagua jukwaa linalowapendeza kufanya siasa zao, na wakati mwingine kuhama kutoka moja kwenda jingine.
Ameeleza kuwa kitendo cha chama hicho kupokea wanachama wapya ni jambo jema kisiasa kwa kuwa hatua hiyo inakiimarisha chama husika.
“Kwa Chaumma kupata wafuasi wapya ni jambo jema kwa chama chochote na kwamba kitajiimarisha,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Kanael, kilichobaki kwa chama hicho ni kuimarisha itikadi yake, kujenga ushawishi na kuhakikisha kinakuwa na rasilimali ili kuwavutia wengi zaidi.
Chaumma wenyewe wanasemaje?
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema baada ya ingizo jipya la wanachama, chama hicho kimefungua ukurasa mpya wa kisiasa, huku akieleza kuwa hata kwenye uchaguzi wa 2025 wanakwenda kushindana na si kushiriki tena.
“Chaumma kinaenda kuwa tumaini jipya kwa ukombozi wa wananchi. Nilikuwa nasubiri kwa muda mrefu jambo hilo, hata kupitia sera yangu ya ubwabwa kwa wote kuanzia asubuhi hadi jioni, sasa ndoto imeanza kutimia,” amesema.
Amesema kupokewa kwa wanachama hao ni mwanzo tu, lakini anaamini ubora wa sera za chama hicho utaendelea kuwa kichocheo na kuwashawishi wengine kujiunga.
“Binafsi nipo tayari kuongoza jahazi hili bila kuwayumbisha na kubeba maono kuelekea kwenye siasa za ushindani. Lakini kubwa zaidi, nataka watu waendelee kujiunga nasi, hasa vijana kwa kuwa wana mvuto na ushawishi mkubwa,” amesema Rungwe.
Rungwe amesema kiu ya Watanzania ni kupata viongozi wenye dira na sera mbadala, na chama chake kina uwezo wa “kupika” watu wa namna hiyo kulingana na Katiba yake.
“Uliona jana wakati tunawapokea wanachama wapya, na tumepata uongozi mpya. Usitazamwe kama kupeana vyeo, bali msingi pale waangalie dhamira yetu ya kutaka kwenda kuwatumikia wananchi,” amesema.
Amesema muda wa kuitwa Chaumma chama cha kawaida umeshapita. Ni zama mpya na itarajiwe chama hicho kinakwenda kushinda viti vingi vya ubunge ili kuwe na mageuzi kwenye vyombo vya uamuzi.